Rais wa Simba sc, Evans Elieza Aveva
WEKUNDU wa Msimbazi Simba juni 29 mwaka huu
wamefanikiwa kupata viongozi wapya watakaoendesha gurudumu kwa miaka minne
ijayo.
Hongera Evans Elieza Aveva kwa kuchaguliwa kwa
kishindo kuwa rais wa kwanza wa Simba kwa kumbwaga kwa mbali mpinzani wako,
Andrew Peter Tupa.
Pia Geofrey
Nyange Kaburu hongera kwa kurudi kwa kishindao katika uongozi wa klabu ya
Simba, safari hii `baba`! unaitwa Makamu
wa Rais na sio makamu mwenyekiti kama siku zile unajiuzulu.
Pia niwape hongera Iddi
Kajuna, Said Tully, Collins Frisch, Ally Suru
Jasmine Badour kwa kuchaguliwa katika nafasi za wajumbe wa kamati ya
utendaji.
Uchaguzi wa Simba sc ulikumbwa na
mizengwe mingi, lakini mwisho wa siku ulimalizika salama.
Evans Aveva tangu uchaguliwe
kuwa rais wa Simba, sijawahi kukueleza lolote, lakini leo hii nimejisikia
kukuambia mambo machache baada ya kuitafakari Simba ya sasa.
Hakuna ubishi, kwa miaka miwili
mitatu, Simba imekuwa ikiwapa machungu mashabiki wake kutokana na matokeo
mabaya ya uwanjani ambayo imekuwa ikiyapata.
Simba imepita katika wakati
mgumu kiuongozi. Migogoro ya ndani kwa ndani imeitafuna kwa muda mrefu.
Uelewano baina ya viongozi haukuwepo na ndio maana mara kadhaa tulisikia
kupinduana.
Hakika mambo yale hayakuwa na
maana katika ustawi wa soka la Simba na Tanzania kwa ujumla.
Simba ni klabu kongwe yenye
mashabiki wengi. Wachache kuiharibu ni kuumiza mioyo ya mamilioni ya watu wengi
walioiweka klabu hiyo kwenye roho zao.
Makamu wa Rais wa Simba sc, Geofrey Nyange `Kaburu`.
Aveva umeingia katika wakati
mgumu ambao Simba ipo katika mpasuko ambao ulisababishwa na uongozi wa Ismail
Aden Rage na baadaye uchaguzi uliokupa ushindi wa kishindo dhidi ya Tupa.
Nafahamu kulikuwa na kambi
mbalimbali wakati wa uongozi, hususani ile ya Michael Richard Wambura
aliyetabiriwa kuwa mpinzani wako mkubwa, lakini alienguliwa na kamati ya
ucghaguzi chini ya mwenyekiti, Wakili Damas Daniel Ndumbaro.
Hizi kambi ni sumu katika
uongozi wako, hivyo ukiwa kiongozi wa juu zaidi katika klabu ya Simba,
unatakiwa kupigana kuzivunja kabisa.
Aveva nakusisitiza ujitahidi
kuvunja makundi hayo kwasababu yatakufanya ushindwe kufikia malengo yako.
Hakuna haja ya kuwachukia wala kuwafikiria vibaya waliokuwa wakikupinga
hadharani.
Moja ya mambo yanayowaathiri
wanasiasa wengi ni kuendeleza chuki baada ya uchaguzi. Kama mtu alikuwa
anakupinga wakati unamwaga sera, haimaanishi ni adui yako.
Mambo ya demokrasia ndivyo
yalivyo. Kupinga na kuunga mkono ni haki ya kila mtu. Haiwezekani na haitawezekana
uungwe mkono na kila mtu. Basi watu hao watakuwa hawafikirii vizuri.
Nilikusikia kwa mara ya kwanza
ukizungumza baada ya kuchaguliwa. Uliweka wazi dhamira yako ya kuvunja makundi.
Nafahamu wakati wa uchaguzi kuna watu walitukanana na kusemana maisha binafsi
na kusababisha chuki za nje ya mpira sababu ikiwa ni wagombea ukiwemo wewe.
Lakini haya yote yanatakiwa
kufutwa ili maisha yaanze kwenda barabara. Aveva wewe ndiye mwenye dhamana ya
kuwezesha hili na unatakiwa kuwa na washauri wazuri juu ya kumaliza tofauti
hizi.
Nategemea uheshimu sera watu
wote waliokuwa wanaomba nafasi, Kuna faida kubwa ya kuongeza ya wenzako
kichwani mwako. Naamini Tupa alikuwa na sera nzuri, lakini wewe umepata nafasi.
Mawazo yake usiyapuuze.
Mashabiki wa Simba sc wanahitaji kushangilia mabao zaidi msimu ujao.
Hata Wambura alikuwa na mawazo
mazuri kwa klabu, japokuwa bahati mbaya wengi walisahau kufikiria mawazo hayo
kutokana na matatizo aliyokuwa nayo. Lakini jaribu kutafakari mawazo yake pia.
Aveva nitafurahi sana kama
utafanya yafuatayo katika uongozi wako:
Mosi; ufanikiwe kujenga uwanja
wa klabu. Kwa muda mrefu Simba haina uwanja. Hii ni historia mbaya kwa klabu
kubwa kama hii. Ndani ya miaka minne unao uwezo wa kuunganisha nguvu ya
wanasimba wote na kufanikiwa kujenga uwanja wa kisasa.
Najua wapo watu wengi nyuma
yako na wana uwezo mkubwa wa kifedha. Kwa kutumia urafiki na nguvu ya uongozi,
jaribu kuwashawishi ili dhamira yako ya uwanja itimie. Umekuwa rais wa kwanza
wa Simba na ukifanikiwa kujenga uwanja, utakuwa Rais wa kwanza kujenga uwanja
wa Simba. Utaingia katika historia ya klabu na kuwa miongini mwa watu wenye
heshima milele.
Naamini zipo jitihada
zinazoendelea huko Bunju katika uwanja wenu, lakini Aveva na wenzako mnao uwezo
wa kufanikisha zaidi.
Ukijenga uwanja katika kipindi
chako cha miaka minne, nitakuwa na la kusema mwaka 2018.
Kocha mkuu wa Simba sc, Mcroatia, Dravko Logarusic akiwa na kikosi chake mwezi desemba mwaka jana.
Pili; Aveva achana na mfumo wa
kuifanya Simba klabu ya kuifunga Yanga tu. Ni kwa muda mrefu sasa, viongozi na
makocha wamekuwa wakitolewa `Kafara` kila wanapofungwa na mtani.
Hili lipo hata kwa Yanga. Ukiwa
kocha wa Yanga, kufungwa na Simba ni hatari katika kazi yako, vivyo hivyo kwa
Simba kufungwa na Yanga ni majanga.
Mserbia, Milovan Circovic
aliwahi kuifunga Yanga mabao 5-0, alionekana kocha bora zaidi japokuwa
aliachishwa kazi. Mfaransa Patric Liewig alionekana kuwa kocha bora, lakini
matokeo aliyoyapa katika mechi za Yanga, yalikuwa na nguvu ya kumuondoa katika
kazi yake.
Hata Abdallah Kibadeni sare ya
3-3 ilichangia kumfuta kazi Msimbazi. Dravko Logarusic aliifunga Yanga mabao
3-1 kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe mwezi desemba mwaka jana na katika mechi
ya marudiano ya ligi kuu soka Tanzania bara alitoka sare ya 1-1.
Matokeo haya kwa kiasi kikubwa
yalichangia kuendelea na kazi yake Simba na kupewa mkataba wa miaka miwili na
uongozi wa Aden Rage.
Ernie Brandts aliwapa Yanga
ubingwa, lakini kipigo cha Nani Mtani Jembe kilifungua balaa kwake kwasababu
alionekana kuwa na kikosi bora na akashutumiwa kuwa timu imeshuka kiwango.
Lakini ukweli ni kufungwa na Simba.
Aveva wakati huu si muda wa
Simba kuiendea Yanga Zanzibar, halafu mechi nyingine inafungwa. Ni muda muafaka
wa kuifanya Simba kuwa klabu ya kisasa na ya ushindani, Tanzania na nje ya
Tanzania.
Tengeneza mkakati wa muda
mrefu. Tengeneza soka la vijana na kuwaamini makocha ili watekeleze mipango
yao.
Najua umechaguliwa kwa kura,
hivyo utaogopa kuwaumiza wapiga kura wako na kutaka kufanya mambo kama
watakavyo, lakini kumbuka mpira una misingi yake. Kuwa na mipango na itekeleze
kwa ueledi mkubwa.
Tatu; Angalia namna ya kuuza
jezi. Kuna mamilioni ya mashabiki wa Simba sc nchi nzima, nembo yenu ni kubwa.
Kuna uwezekano mkubwa wa kuingiza pesa ndefu kupitia jezi zenu. Katika uongozi
wako, fungua maduka ya jezi na vifaa vya Simba. Weka usimamizi mzuri,
nakuhakikishia, utaitoa Simba hapa ilipo.
Nne; dhibiti uwizi wa mapato ya
Simba. Kuna `wahuni` ambao miaka na miaka, Simba ni kitega uchumi kwako. Tafuta
njia ya kuwasaka watu hawa na kuwabaini. Kama utazuia upotevu wa mapato,
utaisaidia Simba kwa kiasi kikubwa. Utaitoa mikononi mwa watu wachache na kuwa
timu ya kujitegemea.
Tano; tafuta washauri wazuri
katika maamuzi yako. Tumeshuhudia viongozi wa ngazi za juu katika vyama vya
mpira wakifanya maamuzi ya kukurupuka. Wengine wanalala na kuamka na maamuzi.
Epuka usanii wa namna hiyo. Tafuta washauri wazuri kwa ajili ya manufaa ya
klabu.
Yapo mengi ya kukwambia Aveva,
Rais Mteule wa Simba. Siku utakayokabidhiwa kijiti rasmi na mhe. Ismail Aden
Rage, nitakueleza kitu.
Vinginevyo, niwapongeze sana wana Simba kwa kufanikisha uchaguzi wenu.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
0 comments:
Post a Comment