Juzi Kamati Kuu ya Simba, chini ya Rais
Aveva, ikifanya Kikao chake cha kwanza, iliamua kuwasimamisha Wanachama
69 ambao waliwasilisha Kesi Mahakamani kutaka kusimamisha Uchaguzi Mkuu
na pia kusema uamuzi wa hatima yao pamoja na ya Michael Wambura,
aliezuiwa kugombea kwenye Uchaguzi huo, utatolewa na Mkutano Mkuu wa
Simba utakaofanyika Agosti 3.
Lakini sasa Wambura ameibuka na kudai
Wanachama hao wana hoja na ndio maana wakaenda Mahakamani na kuruhusiwa
kufungua Shauri lao na hivyo Klabu inapaswa kuwasikiliza.
Wambura alikariri Ibara ya 41 (d) ya
Katiba ya Simba aliyodai inataka Wanachama hao kuitwa na kupewa fursa ya
kujitetea kabla hatua au uamuzi wowote kuchukuliwa dhidi yao.
Kuhusu yeye binafsi, Wambura amedai yeye
suala lake lilimalizwa na TFF kupitia Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi chini
ya Mwenyekiti Julius Lugaziya ambayo ilimrudisha kwenye Uchaguzi Simba.
Wambura alieleza kuwa yeye
ameshasafishwa na Kamati ya Lugaziya na ndio mana alirudishwa kwenye
Uchaguzi huo na kuondolewa tu kwa sababu ya kosa la kufanya kampeni
kabla muda na si vinginevyo na hivyo haoni mantiki ya yeye kupelekwa
kwenye Mkutano Mkuu wa Agosti 3.
Hata hivyo, kiini cha zogo hili la Wambura na Simba inadaiwa ni uhalali wake wa kuwa Mwanachama hai.
Vile vile, Wambura alizungumzia Uchaguzi
wa Simba uliofanyika Bwalo la Maafisa wa Polisi, Oyster Bay, Jijini Dar
es Salaam hapo Juni 29 na kudai Wanachama wengi hawakuridhishwa na
uendeshwaji wake na hivyo hawakubali matokeo.
Wambura alikumbusha kuwa wakati wa
Mkutano huo wa Wanachama wa Uchaguzi, walitangaziwa kuwa idadi ya
Wanachama waliohudhuria ni 2500 lakini kwa upande wa Uchaguzi wa Rais
Kura zilizopigwa zilikuwa 1845 tu ikimaanisha Watu 700 hawakupiga Kura
na hilo limezua shaka na kuibua uhalali wa Uchaguzi huo.
Kwenye Uchaguzi huo, Aveva alitinga madarakani baada ya kuzoa Kura 1455 na kumshinda Andrew Tupa aliepata Kura 388.
KAA CHONJO….sakata linaendelea….
0 comments:
Post a Comment