Afisa
Kata wa Kata ya Mchinga, Bi. Sharifa Mkwango, akisisitiza jambo kuhusu
vijana kujiunga katika vikundi vya uzalizashaji mali.
Vijana
wa Kata ya Mchinga, Lindi Vijijini wakifuatilia kwa makini maelekezo
ya Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Bw. James Kajugusi (hayupo pichani)
wakati akiwaelekeza namna ya kuunda vikundi na kupata mikopo kutoka
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana mwishoni mwa wiki.
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya
Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bw. James
Kajugusi akisisitiza jambo wakati akiwahamasisha vijana wa Mchinga
kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili kuunda SACCOS ya vijana.
Kulia ni Afisa Tarafa ya Mchinga, Bi.Hadija Mringwa.
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Serikali imewataka
vijana Mchinga kushiriki katika shughuli za maendeleo ili kujiinua
kiuchimi na kuleta maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa mwishoni mwa
wiki na Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Bw. James Kajugusi
alipokuwa anaongea na Vijana wa Halmashauri ya Lindi Vijijini Kata ya
Mchinga jana kuhusu masuala ya maendeleo ya Vijana.
Bw. Kajugusi amewaeleza vijana
umuhimu wa kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili kuunganisha
nguvu za kimtaji na kufikiri kwa pamoja namna ya kuboresha maisha yao ya
kila siku.
Vijana wanapokuwa katika vikundi
ni rahisi sana kutambulika nani yuko wapi anafanya nini na anahitaji
nini hivyo kuirahisishia Serikali kuwasadia. Amesema Bw. Kajugusi.
Amesema kuwa kijana wa sasa
anatakiwa kujitambua na kujua kuwa yeye ndiyo tegemeo la taifa hivyo
kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo yeye mwenyewe na taifa
kwa ujumla.
Changamoto kubwa ya vijana ni
kutojitambua hivyo kufikiri kwamba wanahitaji mitaji kwanza wakati bado
hawana hata wazo la kuwekeza na mtaji huo. Amesema Bw. Kajugusi.
Amesema kuwa ni muhimu vijana hao
wakajiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili waweze kuunda SACCOS
yao kwa ajili ya kupata fedha ya mkopo kutoka katika Mfuko wa Maendeleo
ya Vijana ili kukuza mtaji na kuzalisha mali kwa ajili ya maendeleo
endelevu.
Bw. Kajugusi amewaeleza kuwa
kupitia SACCOS ya vijana wataweza kupatiwa mikopo yenye riba nafuu ya
asilimia 10 ya mkopo ambapo asilimia 5 ya riba hiyo inabaki kwenye
SACCOS husika, asilimia 2 inabaki Halmashauri na asilimia 3 inarudi
mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili kuutunisha na kuwawezesha vijana
wengine kukopa.
Aidha, amewataka vijana kujali
afya zao hususan kuepuka matumizi ya dawa za kulevya kwani yanaharibu
akili na viungo vya mwili hivyo kuathiri kiwango cha kufikiri na
kuathiri utendaji kazi na uzalishaji wa kijana.
Halikadhalika, amewataka kujikinga
na magonjwa ya zinaa na mimba za utotoni ili kushiriki kikamilifu
katika shughuli za maendeleo ya jamii.
Naye Afisa Tarafa ya Mchinga, Bi.
Hadija Mringwa aliwataka vijana wa Kata hiyo kuhakikisha kuwa
wanakamilisha zoezi la kujiunga katika vikundi na kuanzisha SACCOS
mapema iwezekanavyo ili waweze kufaidi fursa ya mkopo kutoka katika
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
(Picha zote na Concilia Niyibitanga
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo)
Na Concilia Niyibitanga
0 comments:
Post a Comment