Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete ametaja majina 11 ya
wanachama wa CCM wanaofaa kuwania urais kurithi kiti cha baba yake, Rais
Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake mwakani.
Ridhiwani (35), ambaye alishinda kiti cha ubunge wa Jimbo la Chalinze
Aprili mwaka huu, alitaja majina hayo katika mahojiano maalumu na gazeti
hili yaliyofanyika mjini Dodoma hivi karibuni.
Miongoni mwa aliowataja kuwa wana sifa ni makada watano walio chini ya
uangalizi wa CCM wa mwaka mmoja baada ya kubainika kuanza kampeni za
urais mapema, mawaziri wawili waliopoteza nyadhifa zao katika kashfa ya
Operesheni Tokomeza, mwanamke mmoja na Rais wa Zanzibar.
“Kutaja majina tu, naweza kuorodhesha wengi tu. Naweza kuorodhesha hata
watu 500, kwa sababu tunaona wengi sana,” alisema mtoto huyo wa Rais
Kikwete ambaye amekuwa ndani ya CCM kwa muda mrefu akitokea umoja wa
vijana wa chama hicho, UVCCM. “Kwa mfano, kwa upande wa Bara tunao
Emmanuel Nchimbi, William Ngeleja, January Makamba, Bernard Membe,
Steven Wassira, Edward Lowassa na Asha-Rose Migiro,” alisema.
Aliongeza: “Hawa ni kwa uchache zaidi… ni baadhi ya watu ambao wanatajwa
kwa upande wa Bara, lakini jambo la msingi ni nani mwenye sifa za kuwa
rais.”
Alisema pamoja na kwamba wanasiasa hao wote wanazo sifa za kuiwania
nafasi hiyo ya juu, vikao vya chama ndivyo vitakuwa na nafasi ya
kuwachuja ili kupata wanaotosha. “Kama wanatosha au la, vikao vya chama
vitakaa kuamua licha ya kuwa hao wote niliowataja, kwa sifa za kugombea
urais wote wanajitosheleza. Wana sifa, wana uwezo wa kugombea na wana
uwezo wa kushinda, hao ni kwa upande wa Bara,” alisema.
Alipoulizwa hali ikoje kwa upande wa Zanzibar, Ridhiwani alisema, “Sisi
chama chetu kina utajiri wa watu kwa upande wa Zanzibar kuna Shamsi Vuai
Nahodha, Hussein Ali Mwinyi, Dk Seif Ally Iddi (Makamu wa pili wa Rais
Zanzibar) na Dk Mohammed Ali Shein, Rais wa Zanzibar. Hawa ni watu ambao
wana uwezo na hata wakipewa jukumu la kuongoza nchi hii wanaweza. Tunao
wengi sana.”
Membe, Wassira, Lowassa, Ngeleja na Makamba walipewa adhabu na Kamati ya
Maadili ya CCM ya kutogombea nafasi yoyote ndani ya chama wala kufanya
kampeni baada ya kudaiwa kukiuka taratibu za chama hicho, wakati Nchimbi
na Nahodha walilazimika kujiuzulu nyadhifa zao za uwaziri kutokana na
kashfa ya Operesheni Tokomeza ambayo ililenga kushughulikia majangili,
lakini ikahusishwa na vitendo vya ukiukaji haki za binadamu.
Ridhiwani hakumtaja Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye ambaye pia anatumikia adhabu hiyo ya Kamati ya Maadili ya CCM.
Baadhi kukwama
Hata hivyo, Ridhiwani alidokeza kuwa wapo baadhi ya wanasiasa
watakaokwama kufikia lengo hilo kutokana na kukabiliwa na kesi ndani ya
chama, ambazo hakuzitaja wala kutaja wahusika.
“Kuna watakaopungua kutokana na kesi zinazowakabili katika chama ambazo
zinawafanya wapungukiwe sifa. Kwa maana hiyo kuna watu kama wanne hivi
(wa Bara) unawatoa na ukiwatoa unabakiwa na watatu, sasa unaweza
kujiuliza hao watakaobaki watatu, je, wanatosha?”
Alipotakiwa kueleza iwapo angepewa nafasi ya kuteua mgombea mmoja wa CCM
atakayepambana na vyama vingine katika uchaguzi mkuu mwakani, Ridhiwani
alijibu kwa ufupi kuwa akisema, “Hilo siwezi kujibu.”
Amsaidia Membe
Ridhiwani pia alizungumzia uchaguzi wa ndani ya CCM akikiri kuwa
alimsaidia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Membe
kushinda ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
“Ni kweli katika uchaguzi wa NEC nilimsaidia Bernard Membe. Nilimsaidia
si kwa sababu ya kuwa katika kundi lolote, ila nilimwona kuwa ana sifa
ya kuingia kwenye NEC, hili jambo lazima watu waelewe,” alisema
Ridhiwani.
Hata hivyo, Ridhiwani alieleza kukerwa na kitendo cha baadhi ya wajumbe
ambao katika uchaguzi wa ndani badala ya kufanya kampeni kwa mtu
wanayemtaka, wanafanya kampeni dhidi ya yule wasiyemtaka. “Hili ni jambo
la ovyo ambalo nimewahi kuliona katika chama chetu… na tangu nimezaliwa
sijawahi kuliona. Kwa mara ya kwanza nimekuja kuliona kwenye NEC,”
alisema Ridhiwani ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
“Pale tunagombea nafasi kumi halafu kibaya zaidi ni kwamba watu
wanakampeni ili mtu asipite. Ndiyo maana mimi nikasimama kuwaomba watu
wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani tumsaidie Membe. Walionyesha
ushirikiano wa kutosha na wakamchagua kwa kura nyingi na akaingia NEC.
Mambo ya makundi mimi sina wala siasa yangu haiangalii kundi,” alisema.
Je, atamuunga mkono pia kwenye urais? Ridhiwani anasema: “Hapana. Hiyo
siyo tafsiri sahihi. Naomba niseme jambo moja. Mmoja wa watu
walionipigia kura Chalinze ni baba yangu, japo alisema amempigia kura
mgombea wake, lakini nafahamu kuwa mgombea wake ni mimi kwa sababu
ninatoka katika chama chake, hiyo ni tafsiri ya kawaida kulingana na
maneno yake aliyoyasema.
“Baba yangu aliponipigia kura kuwa mbunge, kesho nitakapogombea nafasi
ya uenyekiti wa CCM wa mkoa, mfano Mkoa wa Pwani halafu akanikataa,
tafsiri haiwezi kuwa baba kamkataa mwanaye.”
Alisema jambo la msingi ni kuwa mtu anatosha katika nafasi gani, hivyo
ikitokea Membe akawa katika nafasi hiyo na ana sifa kuliko wengine
waliojitokeza, atamsaidia katika kuhakikisha anafanikiwa.
“Lakini ikitokea kwamba kuna watu wana sifa zaidi yake hatuwezi
tukakubali kuipeleka hii nchi katika misingi ya kujuana. Tutaangalia
mwenye sifa ni nani,” alisema kwa kujiamini.
Sifa za rais ajaye
Akizungumzia sifa za mtu atakayerithi kiti hicho, Ridhiwani alisema:
“Matamanio yangu ni kumwona rais atakayefuata awe mtu mwenye uwezo wa
kuendeleza pale Bwana Jakaya Kikwete alipoachia. Siyo rafiki yangu,
mchumba wangu wala si mshikaji wangu wala mshiriki wangu katika
baishara. La msingi ni mtu ambaye anaweza.”
Ridhiwani alisema ndani ya CCM kuna watu wengine ambao wana sifa na
uzuri wa CCM haiangalii ni nani amejitokeza bali pia wanaangalia watu
ambao wapo nje ya utaratibu wao, lakini ni makada wazuri ambao hata
wakiletwa, wana sifa za kutosha.
“Ndiyo maana siwezi kujiingiza katika suala la kushabikia nani awe rais.
Tutaangalia ni nani mwenye sifa atajitokeza na nani ambaye tukimuunga
mkono anaweza kututoa hapa tulipo na kutupeleka kuzuri zaidi. Hakuna
urafiki katika suala la nchi, tunaangalia masilahi ya nchi. Siyo
masilahi ya nchi tu, ila masilahi makubwa ya nchi,” alisisitiza
Ridhiwani.
Alisema pamoja na kwamba kwenye vitabu vya mwongozo zimetajwa sifa za
mgombea urais, yeye binafsi akiulizwa sifa za rais anayetakiwa ni kuwa
lazima awe mtu ambaye atakuwa sehemu ya kupata ufumbuzi wa matatizo na
siyo sehemu ya walalamishi.
Alisema mgombea lazima awe mtu ambaye ukimwambia kwamba wananchi hawana
chakula, atakuja na suluhisho ya nini kifanyike, ukimwambia shilingi
imeshuka atakuja na ufumbuzi, akiambiwa kuhusu suala la ajira, atatafuta
ufumbuzi na siyo na yeye kuwa sehemu ya walalamishi.
“Tunamtaka rais ambaye atatambua anaongoza watu gani kwa sababu tuna
tatizo kubwa ambalo ni tishio kwa nchi yetu sasa, mgawanyiko wa madaraja
katika maisha ya watu. Rais lazima ajue anaongoza watu wa namna gani.
Wakati mwingine unakuwa na mtu ambaye anaangalia kundi la watu wake
wanaomzunguka tu, akidhani kuwa ndiyo nchi, rais wa namna hiyo hapana,”
alisema.
Aliongeza: “Rais ninayemtaka anapaswa awe mtu ambaye anaweza kushughulikia mambo yanayogusa maisha ya watu wote.”
“Pia, rais ninayemtaka lazima ajue misingi ya chama chetu. Tuna tatizo
kubwa kwa wanasiasa wetu wa leo wengi hawafahamu nini umuhimu wa
chama…Tuna wabunge wa CCM ndani ya Bunge ambao tangu wameingia bungeni
ni miaka mitano, hawajawahi kuchangia chama.
Alisema katika hali hiyo, anahitajika rais anayefahamu kuwa chama
kinatakiwa kisemewe na demokrasia ya chama lazima iwe kubwa. “Mfano watu
wa CCM wanatakiwa kupewa uhuru wa kusema katika yale ambayo
yanawafurahisha na yale ambayo wanaona hayafurahishi ili ituwezeshe sisi
wanachama kubadilika. Mojawapo ya sifa ya chama ni kubadilika kutokana
na wakati na mazingira ambayo ndiyo moja ya sifa ya chama na chama chetu
sisi kimethibitisha hilo,” alisema.
Ridhiwani alisema ni vizuri apatikane rais ambaye ni muwazi katika
demokrasia na atakayeweza kulinda usalama wa nchi hii kwa sababu nchi
iko katika kipindi kigumu na kiongozi huyo awahakikishie wananchi kuwa
anaweza kutengeneza nyanja mpya za watu kupata ajira.
Ajira 1,000,000 za JK
Ridhiwani, ambaye mwaka 2010 alikuwa mmoja wa wanachama wa CCM waliopewa
jukumu la kuzunguka nchini kutafuta watu wa kumdhamini baba yake ili
apitishwe kugombea tena kiti cha urais, pia alizungumzia ahadi ya Rais
Kikwete ya ajira milioni moja, akisema kuwa imetimia lakini wapo watu
wengine milioni tatu wasiokuwa na ajira.
“Tumeona hapa Rais Kikwete alipokuwa anaingia madarakani alituahidi
ajira milioni moja, lakini mipango ya Serikali ikafungua vyuo vingi, leo
hii ukihesabu ajira milioni moja kwa Serikali zimefika, lakini tuna
wengine milioni tatu bado wapo benchi wanasubiri ajira,” alisema.
Aliongeza kusema: “Sasa tunafanyaje, huyu rais anayekuja lazima atupe
ufumbuzi wa hilo. Siyo ufumbuzi wa kuangalia nyuma kwamba watu
wanaohitaji chakula ni watu kumi, lakini huangalii kumi hao ambao baada
ya kula watazaa, kwa hiyo kesho haitakuwa watu kumi, watakuwa zaidi ya
watu 20.
“Hili ni jambo ambalo kwangu naona ni changamoto ambayo rais anayekuja
lazima alitambue hilo. Pamoja na hilo rais anatakiwa pia awe na uwezo wa
kutambua michango ya wenzake waliotangulia. Siyo shughuli kubwa ya rais
atakayekuja iwe ni kuanza kukosoa wenzake kwamba huyu alifanya jambo la
ovyo; hapana. Afanye kama vile ambavyo waliotangulia wamefanya,”
alisisitiza.
Alitoa mfano wa jinsi marais walivyosahau ya nyuma na kusonga mbele.
“Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alipomaliza muda wake
alipokuja Mwinyi hakuangalia Nyerere alikosea wapi, alichoangalia ni
kuwa nchi inakabiliwa na changamoto gani na tunakwendaje mbele.
“Ametoka Rais Mwinyi, akaja Mkapa ambaye pia aliangalia nchi inakwenda wapi, amekwenda mbele.
Akaja Rais Kikwete ameangalia nchi inakwenda wapi na akaendelea mbele.
Hivyo rais anayefuatia lazima awe na uwezo huo. Aangalie mwenzake
ameishia wapi na aendeje mbele. Yamefanyika mambo mengi nchini, ni
vipaumbele vipi alivyonavyo. Lazima uwe na rais wa namna hiyo.
“Rais ajaye atambue watu katika matabaka yote. Tunao wafanyabiashara,
wacheza muziki, waigizaji wa filamu hivyo lazima rais awatambue na
lazima awe tayari kuwasaidia, atumie nafasi yake kuhakikisha kwamba watu
hawa wanapatiwa haki zao.
“Rais ambaye anakuja lazima atambue watu katika kada mbalimbali. Mfano,
waandishi wa habari wana malalamiko yao, lazima afungue mlango kwa
kukutana nao na azungumze nao ili waseme shida zao kama suala la sheria.
Hapa tunazungumzia muswada wa kuletwa bungeni, hiyo sheria tunafanyaje?
Rais lazima atambue hayo.
“Rais lazima atambue juhudi zinazofanywa na wanamichezo wetu. Jinsi gani
yeye anaweza kushiriki na kusaidia kunyanyua kile kiwango ambacho
michezo yetu imefikia kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya
michezo.”
Kuhusu jimbo lake la Chalinze, Ridhiwani alisema limekaa kwa miaka
mitatu bila mtu wa kuwasemea kwa sababu mbunge wao, Said Bwanamdogo
alikuwa mgonjwa na baadaye kufariki dunia. Hivyo anahitaji kutumia muda
uliosalia kufidia pengo hilo.
“Mimi nimekuja humu ndani (bungeni) lazima nifidie ile miaka mitatu ya
nyuma. Lazima tuikumbushe Serikali kwamba ilikuwa na mipango kadhaa kwa
ajili ya jimbo la Chalinze na kwa nini haijatekelezwa hadi sasa.
Ile ya kuipa nguvu, tunaipa nguvu, zile za kushirikiana tunaangalia jinsi gani tunashirikiana,” alisema.
0 comments:
Post a Comment