Tuesday, 8 July 2014

MBEYA CITY KUINGIA KAMBINI JULAI 15,

  MWAMBUSI APANIA MAKUBWA ZAIDI MSIMU UJAO LIGI KUU

ZIKIWA zimebaki siku sita kabla ya dirisha la usajili kufungwa, benchi la ufundi la Mbeya City limesema liko katika mikakati mikali ya kusajili wachezaji katika nafasi ya kiungo.

Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi amesema yuko katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa viungo wazoefu kabla dirisha la usajili halijafungwa rasmi Julai 15. Mwambusi ambaye ni kocha bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu, amesema kikosi chake hakijaingia kambini Julai 15 kujiandaa kwa msimu ujao wa ligi hiyo.
Juma Mwambusi ameelezea mikakati ya Mbeya City msimu ujao
"Tumefanya usajili wa safu ya ushambuliaji na sasa tatizo tunalo kwenye safu ya kiungo. Tunao viungo wazuri wa kikosi cha kwanza lakini hatuna viungo wa akiba. Kufikia Julai 14 tutakuwa tumeshapata wachezaji wa nafasi hiyo maana tayari tuko katika mazungumzo ya mwisho na wachezaji hao," amesema Mwambusi huku akibainisha kuwa viungo hao wanatoka ndani ya mipaka ya Tanzania. "Tutaingia kambini rasmi Julai 15 lakini bado sijajua tutaweka kambi yetu maeneo gani maana kuna sehemu tatu ambazo zimependekezwa. Kufikia Julai 14 nitakuwa nimeshachagua mahali pa kwenda," amesema zaidi Mwambusi. Amesema kambi hiyo itakuwa ndani ya mipaka ya Tanzania kwa kuwa klabu hiyo haina utaratibu wa kuweka kambi na kusajili wachezaji wa nje ya nchi. Hata hivyo, kocha huyo hakuwa tayari kuyaweka wazi maeneo ambayo uongozi wa timu hiyo umependekeza kwa ajili ya kambi ya timu yake.  Ikiwa chini ya Mwambusi, huku ikishiriki kwa mara ya kwanza VPL, Mbeya City imemaliza nafasi ya tatu msimu huu ikizidiwa kete na mabingwa wapya Azam FC na waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga waliokamata nafasi ya pili. Mbeya City tayari imeshamnasa straika hatari Themi Felix kutoka kwa wakatamiwa wa Kagera, Kagera Sugar.

Na Renatus Mahima, DAR ES SALAAM

Related Posts:

0 comments: