PICHA NA JOHN LUKUWI
Na Anna Nkinda- Maelezo
Mke wa Mfalme wa Swaziland
Malkia Nomsa Matsebula ameipatia shule ya Sekondari ya WAMA- Nakayama
iliyopo kijiji cha Nyamisati wilaya ya Rufiji mkoani Pwani zaidi ya
shilingi milioni tano ili ziweze kuwasaidia wanafunzi wa shule hiyo
katika mahitaji yao ya kila siku.
Malkia Matsebula ambaye ni Mke wa
Mfalme Muswati alitoa fedha hizo jana wakati alipoitembelea shule hiyo
ambayo ni ya bweni inayopokea Watoto yatima na wanaotoka kwenye
familia maskini kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
Akiongea na wanafunzi hao Malkia
Matsebula aliwataka wanafunzi hao kutumia nafasi hiyo kusoma kwa bidii
kwani msichana ni mtu anayeyashika maisha yake ya baadaye katika mikono
yake kwa kujenga nyumba ya upendo, kufanya kazi zake vizuri kwa kuona
jamii yake inakuwa.
Aliwataka kusoma masomo ya aina
mbalimbali ili hapo baadaye waweze kuwa na taaluma mbalimbali zikiwemo
za ujenzi, injinia ,sheria, uhasibu kwani elimu haitoki katika mti bali
ni mpangilio ambao mwanafunzi anajipangia.
“Kumbukeni kuwa Elimu haipatikani
shuleni peke yake bali hata katika jamii inayowazunguka kwani kwenda
shule siyo kama umeelimika bali unatakiwa kuvifanyia kazi vile ambavyo
umejifunza, wanawake onyesheni elimu yenu kwa vitendo ili jamii
inufaike na elimu hiyo.
Wanawake ni watu wanaopenda jamii
ingawa wanakutana na matatizo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ndoa za
utotoni, kuacha shule, unyanyasaji wa kijinsia kwani bila ya wao hakuna
maendeleo katika nchi , nyinyi tumieni nafasi hii kusoma kwa bidii ili
hapo baadaye muweze kuzitatua changamoto hizo”, Malkia Matsebula
alisema.
Aliwasihi wanafunzi hao kujenga
tabia ya kujiheshimu katika maisha yao ikiwa ni pamoja na jinsi ya
kuongea na kuvaa mavazi ya heshima na kuheshimu wengine kwani Elimu
inakuja kwa kujiheshimu.
Aidha Malkia Matsebula aliwaomba
wadau wengine wa maendeleo kumuunga mkono Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
kuwasaidia watoto hao ili waweze kupata elimu jambo ambalo litasaidia
kupatikana kwa viongozi na wanawake wengi wasomi hapo baadaye.
Kwa upande wa walimu aliwataka
kuwafundisha wanafunzi hao Historia ya nchi yao na Bara la Afrika kwa
ujumla ili wajue ni wapi walikotoa na viongozi wao walikuwa wanafanya
mambo gani. Kwa kufanya hivyo wataweza kuilinda na kuitetea nchi na bara
lao.
Naye Mke wa Rais Mama Salma
Kikwete alimshukuru Malkia Matsebula kwa kutembelea shule hiyo na kusema
kuwa tafiti zinaonyesha kuwa kama mtoto wa kike atapata elimu ya
kutosha tatizo la ndoa za utotoni, vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya
watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano vitapungua.
Mama Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ambayo ndiyo
inayoendesha shule hiyo; alisema walichagua elimu kwa mtoto wa kike kuwa
moja ya kazi zinazofanywa na yake kwa kuamini kuwa elimu ni ufunguo wa
maisha ambayo mwanamke alikuwa ameikosa kwa muda mrefu.
“Taasisi ya WAMA iliamua kujenga
shule hii ili kuweza kutoa elimu kwa watoto wa kike ambayo ni yatima
na wanatoka katika mazingira hatarishi kwani watoto hawa walikosa
nafasi ya kusoma ukilinganisha na watoto wengine”, alisema Mama Kikwete.
Shule hiyo ya kidato cha kwanza
hadi cha nne ilianza mwaka 2010 ikiwa na wanafunzi 83 hadi sasa idadi ya
wanafunzi imekuwa na kufikia 336 na katikati ya mwezi huu inampango wa
kuanzisha kidato cha tano na cha sita.
Licha ya kutembelea shule ya
Sekondari ya WAMA-Nakayama Malkia Matsebula aliitembelea Taasisi ya WAMA
iliyopo wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam na kujionea kazi
mbalimbali zinazofanywa na Taasisi hiyo pia alishiriki chakula cha jioni
kilichoandaliwa na mwenyeji wake Mama Salma Kikwete.
0 comments:
Post a Comment