MAKOCHA wa klabu ya FC Barcelona ya Hispania wanatarajiwa kuzuru nchini, imeelezwa.
Kupitia ushirikiano wake na FC Barcelona, bia ya Castle Lager italeta makocha wawili kutoka timu hiyo kuendesha mafunzo maalum ya siku mbili kwa makocha wa Tanzania. Mafunzo hayo yatafanyika kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es salaam tarehe 1 na tarehe 2 Agosti 2014.
Meneja Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania, Fimbo Buttallah, alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari leo kwamba mafunzo hayo yataendeshwa na makocha Isaac Guerrero na Dani Bigas kutoka Shule ya Soka ya FC Barcelona ikiwa ni sehemu ya La Masia ambacho ni chuo bora zaidi cha soka duniani.
Meneja Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Fimbo Buttallah akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu Castle Lager kuwaleta makocha wa FC Barcelona kutoa mafunzo kwa makocha 30 wa ligi kuu na ligi daraja la kwanza. Makocha hao watatoa mafunzo ya siku mbili tarehe 1 na tarehe 2 Agosti kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es salaam. Kushoto ni Meneja wa Castle Lager, Kabula Nshimo
Guerrero hivi sasa ni Mratibu Mkuu wa Shule ya Soka ya FC Barcelona maarufu kama FCB Escola wakati Dani Bigas ni Mratibu wa Mradi wa FCB Escola.
Buttallah alisema “Hii ni fursa ya kipekee kwa makocha wa Tanzania kupata mafunzo maalum ya soka kupitia ushirikiano wa Castle Lager na timu yenye mafanikio makubwa zaidi duniani ikiwa na makocha wenye ujuzi wa hali ya juu. Kupitia mafunzo haya, makocha wa Tanzania watapata fursa adimu ya kujifunza mbinu mbalimbali za mazoezi zinazotumiwa na FC Barcelona”.
Meneja wa Castle Lager, Kabula Nshimo alisema kwamba ushirikiano wa Castle Lager na FC Barcelona umeleta manufaa kwa soka la Tanzania. “Kupitia ushirikiano huu makocha, wachezaji na mashabiki wote watanufaika. Msaada huu wa kiufundi utatoa fursa kwa makocha watakaopata mafunzo haya kuweza kutoa mafunzo yenye ubora kwani makocha hawa wanatumia ujuzi uliozalisha wachezaji kama Lionel Messi”.
Nshimo alisema mafunzo haya yanakuja baada ya mashindano ya Castle Lager Perfect 6 yaliyofanyika nchi nzima na kutoa fursa kwa timu mbalimbali katika kanda sita pamoja na timu ya waandishi wa habari ya TASWA. Wawakilishi hawa wa kila kanda watachuana tarehe 9 Agosti 2014 jijini Dar es salaam wakishindania nafasi ya kwenda kutembelea uwanja maarufu wa Camp Nou unaomilikiwa na FC Barcelona na kuishuhudia timu hiyo ikicheza kwenye uwanja huo nchini Hispania.
Alisema kuwa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) imechagua makocha 30 kutoka Ligi kuu na ligi daraja la kwanza kutoka mikoa mbalimbali kushiriki mafunzo hayo maalum.
Ushirikiano wa Castle Lager na FC Barcelona ulizinduliwa rasmi hapa Tanzania tarehe 17 Agosti, 2013.
Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM













0 comments:
Post a Comment