>>SCOLARI AMWITA MWANASAIKOLOJIA KAMBINI KUSAIDIA WACHEZAJI!
BRAZIL Ijumaa na Jumamosi itashuhudia
Mechi za Robo Fainali za Kombe la Dunia na hii ni kufa na kupona kwa
Nchi 8 zinazogombea Nafasi 4 za Nusu Fainali lakini presha kubwa iko kwa
Wenyeji Brazil ambao walipata kashikashi kubwa kuitoa Chile Raundi
iliyopita kiasi cha baada ya Mechi Kocha wao Luiz Felipe Scolari kumwita
Kambini Mwanasaikolojia lakini habari njema kwao ni kupona kwa Neymar
wakati Kambi ya Belgium, ambayo itaikabili Argentina, mchecheto mkubwa
ni kumzuia Lionel Messi kiasi cha Staa Eden Hazard kupiga mbiu.
SOMA ZAIDI:
Neymar fiti kuikabili Colombia Robo Fainali
Kwenye Mechi iliyopita, Brazil
walipoitoa Chile kwa Penati baada ya kutoka Sare 1-1 katika Dakika 120,
mara mbili Neymar alilazimika kutoka nje kutibiwa baada kugongwa kwenye
Goti na Pajani.
Neymar ndie aliefunga Penati iliyowapa ushindi Brazil lakini alimaliza Mechi hiyo akiwa na michubuko na uvimbe.
Akiongea baada ya kumaliza Mazoezi
kwenye Kambi ya Brazil huko Teresópolis, Neymar alisema: “Nitaweza
kucheza na Colombia. Sisikii maumivu. Nimekuwa nikifanya Mazoezi vizuri.
Hamna wasiwasi.”
Luiz Felipe Scolari amwita Mwanasaikolojia Kambini
Bosi wa Brazil Luiz Felipe Scolari
amemwita Mwanasaikolojia Kambini mwa Timu yake mara baada ya Mechi yao
iliyopita waliyoitoa Chile kwa Penati baada ya kutoka Sare 1-1 katika
Dakika 120.
Baada ya Mechi hiyo, Wachezaji kadhaa wa Brazil walionekana wakibubujikwa machozi walipokuwa wakisheherekea ushindi wao.
Mmoja wa Wachezaji hao alikuwa Neymar
ambae amekiri Gemu hiyo na Chile iliwapa msisimko lakini amekataa kwamba
Kikosi chao kimetingwa na mawazo.
Hata hivyo, hatua hii ya Scolari ya
kumtumia Mwanasaikolojia ni mbinu dhahiri ya kuwapunguzia presha
Wachezaji wake ambao wamebeba zigo zima la kuwa Wenyeji wa Kombe la
Dunia wanaotakiwa kutwaa Kombe hilo.
Akijizungumzia binafsi, Neymar, ambae
ndie anaonekana aliebeba zigo zito na ambae ameifungia Brazil Bao 4 hadi
sasa, ameeleza: “Sijisikii mzigo wowote wa kuwekwa mbele. Ninao
wenzangu kwenye Timu wanaonisaidia. Wengine hupokonya Mipira,
wenginehutoa pasi, wengine hufunga. Sisi ni Timu!”
Hazard: ‘Lazima tumsimamishe Messi!’
Katika Mechi zao zote 4 walizocheza huko
Brazil, Argentina, chini ya Kocha Alejandro Sabella, wameshinda baada
ya mchango mkubwa wa Messi.
Hazard amesema kumdhibiti Messi kutawasaidia sana wao kushinda.
Ametamka: “Tunajua wana Mchezaji Bora
Duniani kwenye Timu yao, lakini hatuogopi. Tunaweza kushinda. Argentina
wamefanya vizuri lakini wanae Mchezaji mmoja ambae ndie huwaletea
tofauti katika kila Mechi. Tukimzuia, tuna nafasi, lakini si rahisi.”
Pia, Hazard amesema wana matumaini
makubwa ya kuifikia Rekodi ya Timu yao ya Taifa ya Mwaka 1986 ambayo
ilifungwa kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Dunia.
0 comments:
Post a Comment