Tuesday, 8 July 2014

KOMBE LA DUNIA: FIFA YADAIWA KUZUIA MAREFA ‘UKALI’, ‘MADAWA’ POA!


>>MARADONA NDIE WA MWISHO KUBAMBWA ‘MADAWA MARUFUKU’ MWAKA 1994!
REFA-DRACULAFIFA imekanusha taarifa za kwamba imewaagiza Marefa wanaochezesha Kombe la Dunia kutotoa Kadi Nyekundu na Kadi za Njano ili kufanikisha Fainali ziwe za raha zaidi na pia imethibitisha hadi sasa hakuna Mchezaji aliebambwa kutumia ‘Madawa Marufuku.’
SOMA ZAIDI:
MAREFA
FIFA imekanusha taarifa kwamba imewaagiza Marefa wanaochezesha Kombe la Dunia kutotoa Kadi Nyekundu na Kadi za Njano ili kufanikisha Fainali ziwe za raha zaidi.
Habari hizo zimezuka kutoka huko Germany ambako, pamoja na Kambi ya Timu yao huko Brazil, wameshika Mabango kuhusu Marefa kuipendelea Brazil hasa wakijua Leo hii Nchi yao inaivaa Brazil kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Dunia.
Gazeti la Germany, Bild, liliripoti kuwa Mkuu wa Marefa wa FIFA, Massimo Busacca, amewaagiza Marefa kutotoa Kadi nyingi ili kuongeza ladha ya Mchezo lakini Msemaji Mkuu wa FIFA, Walter De Gregorio, amechukizwa na habari hizo.
Amesema: “Hiyo Stori kwamba FIFA ina mipango ya siri, Marefa kutotoa Kadi za Njano na Nyekundu ili kuongeza ladha…kwa maneno mengine, FIFA inahatarisha na kukubali Wachezaji kama Neymar na wengine kuumizwa. Hili halikubaliki.”
Wajerumani hao wameishikia bango Mechi ya Brazil na Colombia, ambayo Neymar aliumizwa vibaya na kumfanya akose Mechi zilizobaki za Kombe la Dunia, kwamba ndio Mechi iliyokuwa na Rafu nyingi, Rafu 31, na kuzidi Mechi nyingine zote za Fainali za Kombe la Dunia tangu Mwaka 1966 Takwimu zilipoanza kukusanywa.
Pia, Takwimu zimeonyesha Wastani wa Kadi za Manjano za Fainali hizi ni 2.8 kwa Mechi ukilinganisha na 3.8 Fainali za 2010 na 4.8 zile za 2006.
De Gregorio amesema: “Hiyo ni sehemu ya mchezo na tunaikubali. Lakini tusichokubali ni swali la maadili, kwamba kuna njama za FIFA! Hilo linaingia kabisa kwenye chimbuko la FIFA..la kuwalinda wahusika wakuu, Wachezaji, ambacho ni kitu muhimu kabisa kupita yote!”
Aliongeza: “Lazima tulinde Wachezaji. Ikiwa Neymar hachezi Nusu Fainali au Fainali, hii sio nzuri kwetu!”
FIFA- WACHEZAJI SAFI ‘MADAWA MARUFUKU’
FIFA imetoboa kuwa kila Mchezaji aliepimwa utumiaji ‘Madawa Marufuku’ amekutwa safi baada ya Vipimo zaidi ya 1,000 kuchukuliwa kwenye Fainali za Kombe la Dunia huko Brazil.
Taarifa hizo zimetangazwa na Kamati ya Afya ya FIFA huko Brazil hapo Jana.MARADONA
Jiri Dvorak, Daktari Mkuu wa FIFA, amewaambia Wanahabari huko Maracana, Rio de Janeiro hapo Jana, kuwa kila Mchezaji wa Timu zote 32 zilizoshiriki Fainali za Kombe la Dunia, ikiwa ni Jumla ya Vipimo 736, alitoa Damu na Mkojo ili zipimwe.
Dvoraka alisema, kati ya Machi Mosi na Juni 11, kabla Fainali kuanza huko Brazil, walichukua Vipimo 777 vya Wachezaji pamoja na vingine 232, yaani Vinne toka kila Mechi katika Mechi 58 za kwanza, baada Mashindano kuanza hapo Juni 12 na vyote vilitoa majibu kwamba hamna matumizi ya ‘Madawa Marufuku’.
FIFA imetamka kuwa Mechi 4 zilizobaki, yaani Nusu Fainali mbili, ile ya kugombea Mshindi wa Tatu na Fainali yenyewe, pia zitafanyiwa Vipimo vya kustukiza kwa kulenga Mchezaji yeyote na Matokeo kutolewa kabla ya Mechi inayofuata.
Vipimo vyote vya Wachezaji hurushwa kutoka Brazil na kupelekwa Switzerland kwenye Maabara ya WADA, World Anti-Doping Agency, Kitengo cha Kupinga Matumizi ya Madawa Marufuku, kufanyiwa uchunguzi.
Mara ya mwisho kwa Mchezaji kubambwa akiwa ametumia ‘Madawa Marufuku’ ni kwenye Fainali za Mwaka 1994 huko USA ambako Staa wa Argentina, Diego Maradona, aligundulika na kufukuzwa na kufungiwa.

Related Posts:

0 comments: