KOCHA wa mazoezi ya
viungo wa Yanga, Mbrazili Leonardo Neiva, jana Ijumaa aliwafanyisha
mazoezi ya maana makipa, Juma Kaseja na Ally Mustapha ‘Barthez’, kiasi cha
wawili hao kutikisa vichwa na kukubali muziki wa Kibrazili.
Neiva ambaye ana nguvu
za miguu kama mchezaji anayecheza Ligi Kuu, alikuwa akiwapigia makipa hao wa
Yanga mashuti makali golini akilenga katika kingo za magoli hayo kitendo
ambacho kiliwapeleka mchakamchaka makipa hao na kushindwa kuokoa michomo mingi.
Awali Kaseja na Barthez
pamoja na kipa wa kikosi cha vijana cha Yanga, walikuwa wakipewa mafunzo ya
kawaida na kocha wa makipa, Juma Pondamali, lakini Neiva aliingilia kati na
kumwomba Pondamali awape funzo la maana makipa hao.
Akizungumza na
Mwanaspoti mara baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Neiva alisema:
“Nimejitahidi kuwapigia mashuti japo sijaweza sana kutokana na maumivu ya goti,
nashukuru Kaseja na Barthez wanaonyesha mwelekeo, si rahisi kudaka mashuti yote
lakini wamefanya vizuri.”
Chanzo: Mwanaspoti
0 comments:
Post a Comment