Jamii imetakiwa kushirikiana kwa
pamoja kupiga vita ndoa za utotoni hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha
kuwa sera na sheria za kuwalinda watoto zinafuatwa ili watoto wa kike
waweze kusoma na kumaliza masomo yao kama ilivyo kwa watoto wa kiume.
Mwito huo umetolewa jana na Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na viongozi na Asasi za kiraia
kutoka nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara wanaohudhuria mkutano
wa mwaka wa siku nne wa Taasisi ya Familia ya SEGAL unaofanyika katika
Hoteli ya Ngurdoto mjini Arusha.
Mama Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema ndoa za
utotoni ni moja ya sababu inayowafanya watoto wa kike kutomaliza masomo
yao kwani idadi ya wanafunzi wa kike walioko shule ya msingi ni kubwa
lakini katika elimu ya Sekondari idadi yao inapungua ukilinganisha na
watoto wa kiume.
“Tafiti mbalimbali zilizofanyika
zinaonyesha kuwa katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika asilimia
24 ya wasichana wanaolewa wakiwa na umri mdogo wa kati ya miaka 15 hadi
18, kwa umri huu watoto hawa wanatakiwa kuwa shule za Sekondari na siyo
kuishi maisha ya ndoa wakiwa wameolewa.
Kutokana na sababu hii tunatakiwa
kuunganisha nguvu zetu ili kuhakikisha katika nchi zetu kuna sera na
sheria ambazo zitawalinda wasichana wadogo dhidi ya wanaume wabaya,
wakati huo huo tunatakiwa kushirikiana na jamii ili iweze kuwajengea
mazingira mazuri na salama ambayo yatawalinda watoto hawa”, alisema Mama
Kikwete.
Aidha Mama Kikwete alisema mkutano
huo umekuja wakati muafaka kwani nchi nyingi zinakabiliwa na changamoto
ya maambukizi makubwa ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) miongoni mwa vijana .
Kazi kubwa imefanywa ili kuhakikisha maambukizi ya ugonjwa huo
yanapungua ila hata hivyo bado kuna vijana wengi ambao hawafikiwi na
hudumu muhimu wanazozihitaji .
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema,
“Ugonjwa huu bado ni tatizo katika nchi zetu kati ya maambukizi mapya
620,000 yanayotokea kila mwaka barani Afrika kwa vijana wenye umri wa
kati ya miaka 15 hadi 24 asilimia 60 ni wasichana. Hii inamaana kuwa kwa
kila saa moja wasichana 31 wanapata maambukizi kwa kila vijana wa
kiume 21 tunahitajika kufanya jambo la ziada hasa kwa wasichana ili
kukabiliana na jambo hili.
Vijana wanatakiwa kufundishwa afya
ya uzazi ili waweze kujilinda na kuweza kufanya maamuzi sahihi kuhusu
miili yao hii ni moja ya silaha ambayo itawalinda wasichana. Najua
katika jamii nyingi ni vigumu kwa wazazi kuongea jambo hili na watoto
wao na kuona kuwa ni mwiko, naamini muda umefika kuangalia tamaduni hizi
kwani watoto wengi wanapoteza maisha kutokana na jamii kukaa kimya”, .
Alisema wao kama wazazi
hawatakubali kuona watoto wao wanajihusisha na mahusiano ya kimapenzi
wangali wadogo, wanapata mimba wakiwa na umri mdogo na kukatisha masomo
yao kwani ni wajibu wao kuwalinda dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na
kuhakikisha kuwa hawapati maambukizi ya Ukimwi.
Kwa upande wake mwanzilishi wa
Taasisi hiyo Barry Segal alimpongeza Mama Kikwete kwa kazi kubwa
anayoifanya ya kuwasaidia wanawake na watoto wa Tanzania na kumuahidi
kuwa watashirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa matatizo
yanayowakabili yanapungua au kuisha kabisa.
Alisema Taasisi hiyo imeamua
kufanya kazi na WAMA ili kuhakikisha kuwa kampeni ya Mtoto wa Mwenzio
ni Mwanao inatekelezwa hapa nchini hii itasaidia jamii kuwajengea
mazingira ya kuwalinda vijana wenye umri wa kati ya miaka 14 hadi 24 na
kuwalinda na mazingira hatarishi ambayo yanaweza kuwapelekea kupata
maambukizi ya VVU na hivyo kupata kizazi kisicho na maambukizi .
Taasisi ya Familia ya SEGAL ambayo
makao yake Makuu yapo nchini Marekani wanashirikiana na kufanya kazi na
Asasi mbalimbali za Kiraia zinazofanya kazi za kijamii ikiwa ni pamoja
na kuwawezesha wanawake, kupiga vita mimba za utotoni zilizopo nchi za
Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania.
Na Anna Nkinda – Maelezo, aliyekuwa Arusha
0 comments:
Post a Comment