Mh Pinda
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi za kwanza
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuingia kwenye ubia na sekta binafsi
katika mradi mkubwa wa usafirishaji abiria.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne,
Juni 3, 2014) wakati akifungua Mkutano wa Majadiliano yenye lengo la
kuutangaza mradi wa mabasi yaendayo kasi kwenye ukumbi wa Mlimani City.
Mkutano huo wa siku mbili, utamalizika kesho (Jumatano, Juni 4, 2014).
Waziri Mkuu amesema kutèkelezwa kwa
mradi huo kutatoa fursa za ubunifu utakaowezesha kupatikana kwa
suluhisho la usafiri mijini na hasa kwenye miji inakua kwa kasi barani
Afrika.
"Mbali ya kutoa huduma za hali ya juu,
za haraka na ambazo siyo ghali kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, nia
ya Serikali ni kuona mfumo mpya wa matumizi ya kadi kwenye mpango huu wa
usafiri unatumika ipasavyo," alisema.
Alisema ni matumaini ya Serikali kwamba
wadau kutoka sekta binafsi ambao ni wazawa na wa kutoka nje ya nchi
watashiriki kwenye mradi huu ili uweze kuboresha matumizi ya kadi ambayo
mtu hatatakiwa kulipia fedha taslimu akiwa ndani ya basi bali kutumia
kadi anayoilipia kabla ya kuingia ndani ya basi husika.
Akizungumza na waandishi wa habari mara
baada ya kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema Serikali iliamua
kuanzisha mradi huo ili kupunguza msongamano wa magari kwenye barabara
za Jiji la Dar es Salaam.
"Hii ni awamu ya kwanza ambayo
inakaribia kukamilika na inaanzia Kimara hadi Kivukoni na itakuwa na
matawi mawili ya Morocco na Karikoo. Mradi wote una awamu sita za ujenzi
kuelekea maeneo tofauti ya Jiji," alisema.
Mbali na mradi huo wa mabasi yaendayo
kasi, Serikali inaangalia uwezekano wa kutumia usafiri wa majini kwa
kutumia boti kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo kama njia mojawapo ya
kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.
“Vilevile tutaimarisha usafiri wa reli
kama njia nyingie ya kupunguza tatizo hili. Dk. Mwakyembe (Waziri wa
Uchukuzi) ameanza na sote tumeona ni jambo linalowezekana. Cha msingi ni
kuimarisha tu usafiri huu,” aliongeza Waziri Mkuu.
Mapema, akiwakaribisha wajumbe wa
mkutano huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bibi Hawa
Ghasia alisema Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa mradi huo
unafanikiwa.
Pia
alitumia fursa hiyo kuishukuru Benki ya Dunia ambayo alisema imetoa
kiasi cha dola za Marekani milioni 200 kwa ajili ya kufadhili mradi huo.
Mkutano huo unawashirikisha wadau
mbalimbali wakiwemo wa ndani na wa nje wanaotarajiwa kutoa huduma za
mabasi makubwa na madogo, utoaji tiketi, ulinzi, usafi na huduma za
maduka.
0 comments:
Post a Comment