Thursday, 5 June 2014

KAMATI YA RUFANI YA UCHAGUZI KUKETI JUNI 9

Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inakaa Jumatatu (Juni 9 mwaka huu) kusikiliza rufani moja inayopinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba.

Michael Wambura amewasilisha rufani yake TFF akipinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba iliyomwengua katika kinyang’anyiro cha kuwania urais katika uchaguzi wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Kamati hiyo inayoongozwa na Wakili Julius Lugaziya itakutana saa 5 asubuhi kwenye hoteli ya Courtyard iliyopo Upanga, jijini Dar es Salaam.

NYOTA WAWILI COPA WAENDA BRAZIL
Wachezaji wawili waliochaguliwa kwenda kwenye kambi ya Copa Coca-Cola ya Dunia nchini Brazil wamekabidhiwa bendera tayari kwa safari hiyo inayofanyika leo (Juni 4 mwaka huu).

Hafla ya kukabidhi bendera hiyo kwa Ali Shabani Mabuyu na Juma Yusuf imefanyika leo katika hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam. Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juliana Yassoda ndiye alikabidhi bendera.

Wakati Mabuyu kutoka Ilala alikuwa mchezaji bora wa michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 kwa mwaka 2013/2014, Yusuf kutoka Zanzibar ndiye aliyeibuka mfungaji bora katika michuano hiyo.

Wachezaji hao watakuwa katika kambi hiyo itakayokuwa katika Jiji la Sao Paulo kwa siku kumi ambapo watafundishwa masuala mbalimbali ya mpira wa miguu. Pia watashuhudia mechi ya ufunguzi ya Fainali za Kombe la Dunia katika ya wenyeji Brazil na Croatia itakayochezwa Juni 12 mwaka huu.

BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

0 comments: