Ushirikiano wa pamoja unatakiwa
baina ya wanafunzi, walezi, wazazi, jamii na walimu ili kuweza kujenga,
kuimarisha na kukuza nidhamu , mwenendo na tabia ya mtoto jambo ambalo
litaleta mafanikio chanya pamoja na kutatua changamoto za kitaaluma na
kimazingira.
Hayo yamesemwa jana na Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na walimu pamoja na wanafunzi
wa shule ya Sekondari Salma Kikwete iliyopo kata ya Kijitonyama wilaya
ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema nidhamu ya
mwanafunzi siyo tu kumuamkia mwalimu bali pia kujua wajibu wake kama
vile kuwahi shuleni, kufanya mazoezi ya darasani na kusoma kwa bidii.
“Neno nidhamu lina dhana pana
kwani linagusa wengi lakini katika mazingira ya leo walengwa wakubwa
ni mzazi,mlezi au jamii, mwalimu na mwanafunzi. Kazi ya mzazi, mlezi na
jamii ni kuhimiza na kufuatilia maendeleo ya mtoto.
Mwalimu kufundisha, kuingia
darasani kwa wakati na kujiandaa na kwa mwanafunzi ni kupokea maarifa
anayopewa na mwalimu wake na kusoma kwa bidii”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wa wanafunzi aliwasihi
kuongeza juhudi katika masomo na kufanya vizuri kwenye mitihani, kwani
wao na wengine wote wanategemewa na familia, jamii zao na taifa kwa kuwa
watakuwa wakombozi siku za baadaye na kumuomba Mwenyezi Mungu awape
nguvu na ujasiri katika safari yao ndefu ya kufatuta elimu.
Aidha Mama Kikwete aliwapongeza
walimu wa shule hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya uboreshaji wa elimu
pamoja na kukabiliwa na changamoto kadhaa lakini kadri siku
zinavyokwenda mbele ndivyo Serikali inavyozidi kutatua changamoto
mbalimbali zinazowahusu walimu.
Mwenyekiti huyo wa WAMA
alisisitiza, “Walimu timizeni wajibu wenu kwa kufika kazini mapema,
kumaliza silabasi kwa wakati, kukamilisha maandalio ya masomo,
kufundisha kila kipindi bila kukosa, kujua taarifa na udhaifu wa
wanafunzi wenu na kuwa kiungo kati yenu na wazazi au walezi hiyo ndiyo
nidhamu ya mwalimu na ndiyo ualimu”.
Akisoma taarifa ya shule hiyo
Mwalimu Elestina Chanafi alisema shule hiyo ilianza mwaka 2007 ikiwa na
wanafunzi 320, walimu 13 na vyumba vya madarasa sita hivi sasa ina
wanafunzi 1229, walimu 33 na vyumba vya madarasa 22. Hadi sasa jumla ya
wanafunzi 1161 wamehitimu masomo yao tangu walipoanza kutoa kidato cha
nne mwaka 2010.
Mwalimu Chanafi ambaye ni Mkuu wa
shule hiyo alisema wamefanikiwa kuchimba kisima cha maji kwa msaada wa
wakorea, kuunganisha umeme, kununua vifaa mbalimbali vya uchapaji na
udurushaji, kuboresha mazingira kwa kiwango cha kutia moyo na
kuweza kuwavutia wanafunzi ili wajisikie kuwa sehemu ya shule.
Kuanzisha maabara ya muda ambayo
imewawezesha wanafunzi wa sayansi kufanya mitihani kwa vitendo na
kuongeza kiwango cha ufaulu kwa masomo hayo na kupata wanafunzi wa
kujiunga na masomo ya ngazi ya juu kwa idadi nzuri.
“Changamoto zinazotukabili ni
uchakavu wa baadhi ya vyumba vya madarasa, mmomonyoko mkubwa wa maadili
ambao unasababisha ugumu katika kudhibiti nidhamu ya wanafunzi, uelewa
mdogo wa wazazi juu ya mchango wao kwa maendeleo ya wanafunzi, kiwango
kidogo cha ruzuku toka Serikalini ambacho hakiletwi kwa ukamilifu na
wakati, ufinyu wa bajeti na ulegevu wa uchangiaji wa ada na michango
mingine toka kwa wazazi”, alisema Mwalimu Chanafi.
Naye Mkuu wa wilaya ya Kinondoni
Jordan Rugimbana alimshukuru Mama Kikwete kwa kupata nafasi ya
kuitembelea shule hiyo na kumpongeza kwa kazi anayoifanya ya kuinua
kiwango cha elimu nchini na kuendeleza fani yake ya ualimu kwa faida ya
kizazi cha leo na kijacho kwa kuwasomesha watoto zaidi ya 600 hawa ni
mbali na wanafunzi walioko Shule ya Sekondari WAMA-Nakayama iliyopo
wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Mama Kikwete aliichangia shule
hiyo mifuko 100 ya simenti ambayo itatumika kuzima mashimo katika
vyumba vya madarasa ambapo wilaya ya Kinondoni itagharamia mchanga
pamoja na kumlipa fundi atakayefanya kazi hiyo.
Habari Na Anna Nkinda – Maelezo
0 comments:
Post a Comment