Mbunge wa
Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amewataja kwa majina mawaziri
na wabunge aliosema bungeni kuwa wamekuwa ombaomba katika mifuko ya
hifadhi ya jamii.
Baadhi ya
waliotajwa ni pamoja na Mbunge wa Kongwa ambaye pia ni Naibu Spika, Job
Ndugai; Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge),
William Lukuvi; Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki na
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana na
wabunge Betty Machangu (Viti Maalumu), Livingstone Lusinde (Mtera), John
Komba (Mbinga Magharibi), Eugen Mwaiposa (Ukonga) na Gudluck Ole Medeye
(Arumeru Magharibi).
Hata
hivyo, gazeti hili halijawataja majina mawaziri na wabunge wengine
waliomo kwenye orodha hiyo ya Lissu kwa kuwa hawakupatikana jana kujibu
tuhuma hizo.(Martha Magessa)
Mbali na
kuwataja kwa majina, Lissu pia ametoa vielelezo vinavyoonyesha jinsi
walivyokuwa wakiidhinishiwa malipo kwa nyakati tofauti na Mfuko wa
Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF), kwa sababu
mbalimbali.
Lissu
alimwambia mwandishi wetu jana kuwa licha ya kiwango cha fedha kutokuwa
kikubwa, lakini kinaweza kusababisha mgongano wa kimasilahi kati ya
wajibu wa wabunge kwa umma na masilahi yao binafsi.
"Hali hii
inaweza kusababisha Bunge likashindwa kutimiza wajibu wake wa kikatiba
wa kuisimamia Serikali na taasisi zake," alisema Lissu huku akisisitiza
azimio lake la kuwasilisha hoja binafsi kwa Spika wa Bunge ili iundwe
tume kuchunguza suala hilo.
Mkurugenzi
Mkuu wa LAPF, Eliud Sanga jana alikiri kuwa shirika hilo liliidhinisha
malipo kwa mawaziri na wabunge hao kwa ajili ya shughuli mbalimbali za
maendeleo.
Hata
hivyo, alisema shirika hilo halitoi fedha taslimu, bali hununua vitu
ambavyo viliombwa na viongozi hao kwa ajili ya kusaidia wananchi na si
kufanya biashara.
Sakata lenyewe
Akizungumzia
jinsi mawaziri na wabunge hao walivyosaidiwa, Lissu alisema LAPF ilitoa
Sh2.5 milioni kwa ajili ya mradi wa madarasa Jimbo la Kongwa
linaloongozwa na Ndugai.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Ndugai alisema hakuna tatizo lolote kwa mbunge kupewa msaada na mfuko wa kijamii.
"Huyo
Lissu ana upungufu mkubwa. Hivi LAPF ikisaidia Sh2 milioni kwa ujenzi wa
darasa unaogharimu Sh10 milioni ni tatizo hilo? Nchi hii inakwenda wapi
jamani, siyo kila kitu wanachozungumza wapinzani ni hoja, kama LAPF
wangekuwa wanatoa fedha lingekuwa tatizo lakini wanasaidia vifaa tu."
CHANZO:MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment