Meneja
Mawasiliano wa TANAPA Pascal Shelutete akizungumza na wanahabari jijini
Arusha alipokuwa akitangaza Wanahabari waliofika fainali ya TUZO ZA
HABARI ZA TANAPA ZA MWAKA 2013 wanaotarajiwa kukabidhiwa tuzo zao wiki
ijayo jijini Mwanza wakati wa Mkutano wa kila mwaka wa TANAPA na
Wahariri wa Habari nchini.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jumla ya Waandishi wa Habari 10
wamefanikiwa kufikia hatua ya fainali ya Tuzo za Uandishi wa Habari za
Shirika la Hifadhi za Taifa za mwaka 2013.
Wanahabari waliofanikiwa kufika
hatua ya fainali ni pamoja na Frank Leonard (Habari Leo), Jackson
Kalindimya (Nipashe), Humphrey Mgonja (Radio SAUT FM), Raymond
Nyamwihula (Star TV) na Vedasto Msungu (ITV).
Wengine ni pamoja na Kakuru Msimu
(Star TV), Gerald Kitabu (The Guardian), Salome Kitomari (Nipashe),
David Rwenyagira (Radio 5) na Cassius Mdami (Channel Ten).
Hafla ya utoaji Tuzo za Habari za
TANAPA itafanyika siku ya Jumanne tarehe 27 Mei, 2014 jijini Mwanza
ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.
Lazaro Nyalandu.
Hafla hii itaenda pamoja na
Mkutano wa kila mwaka baina ya TANAPA na Wahariri wa Habari kutoka
vyombo mbalimbali vya habari nchini inayotarajiwa kuanza wiki ijayo
jijini Mwanza.
Jumla ya kazi zilizotumwa kwa
ajili ya kushindanishwa mwaka huu ni 114 tofauti na kazi 34 za mwaka
jana. Ongezeko hili la asilimia 235 lililazimu Jopo la Majaji kutumia
muda mwingi zaidi wa kupitia kazi zote na kupata washindi. Kati ya kazi
114 zilizotumwa, kazi zilizohusu Uhifadhi ni 64 (sawa na 56%) na kazi
zilizohusu Utalii wa Ndani zilikuwa 50 (sawa na 44%).
Tuzo za Uandishi wa Habari za
TANAPA hutolewa kila mwaka kwa nia ya kuwashirikisha wanahabari
kushindanisha umahiri wa kazi zao katika kuelimisha jamii umuhimu wa
dhana ya Uhifadhi kwa maeneo yaliyotengwa kisheria kama Hifadhi za Taifa
na uhamasishaji wa Utalii wa Ndani kwa faida ya uchumi wa nchi yetu.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
Hifadhi za Taifa Tanzania
23.05.2014
0 comments:
Post a Comment