Na Miza Kona – Maelezo Zanzibar
MAKAMU wa Pili wa Rais Balozi Seif
Ali Idd amewataka viongozI kuacha uchochezi wa migogoro ya ardhi
baina ya wananchi na wawekezaji kwa lengo la kujipatia manufaa yao .
Wito huo ameutoa huko Baraza la
Wawakilishi Chukwani wakati alipokuwa akifanya majumuisho ya majadiliano
ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa Fedha 2014/2015.
amesema kuna baadhi ya viongozi
wanawachochea wananchi kufanya migogoro kwa sababu za kisiasa kitendo
ambacho kinapelekea kukosa maendeleo ya nchi.
“Tuache kuchochea wananchi kufanya
migogoro,pia tuache kuchochea wananchi na wawekezaji kwa lengo la
kuleta maendeleo ya nchi ili serikali ipate pato na wananchi wapate
ajira na kukuza uchumi”, alifahamisha Balozi Seif.
Balozi Seif amewasisitiza viongozi
kuwashajihisha wananchi kuleta maendeleo na kuepuka Uchochezi wa
kisiasa kwa lengo la kukuza uchumi ili jamii iweze kuhamasika na
kudumisha amani.
Aidha Makamo wa Pili wa Rais
amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa siasa kutaja Majina ya viongozi
wanapokuwa katika majukwaa ya kisiasa badala yake wanadi sera za vyama
vyao.
Amesema viongozi wanapokuwa katika
majukwaa ya siasa wanatakiwa kuwaelimisha wananchi mambo ya maendeleo
ya nchi na sio kujadili kwa kuwataja majina watu kwani kufanya hivyo ni
kuhatarisha amani na utulivu uliopo.
“Ili amani na utulivu iendelee
nchini basi ni lazima wanasiasa kuachana na tabia ya kujadili na
kutajana majina ya watu katika majukwaa ya siasa, mnatakiwa kukaa kwenye
majukwaa kunadi sera za vyama na kuwaelimisha wananchi jinsi ya kuleta
maendeleo ya nchi”, alisisitiza Balozi Seif.
Aidha Makamo huyo amefahamisha
kuwa fedha za serikali zinatumika ipaswavyo kama zilivyopangwa kinyume
na baadhi ya watu wanavyodai kuwa zinatumika kinyume na mahitaji
yaliyopangwa.
Mapema akifanya majumuisho hayo
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohammed Aboud Mohammed
amewataka wajumbe hao kushirikiana kwa pamoja na kuachana na malumbano
ili kuweza kuimarisha uchumi wa nchi.
Aidha amefahamisha kuwa ni vyema
kuimarisha Muungano na kujadili mambo ya msingi kwa kuondoa kero
zilizopo kwa kujenga hoja zitakazopelekea kupatikana Katiba bora.
Wajumbe hao wameipitisha vifungu
vya bajeti ya Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais kwa mwaka fedha 2014/2015
kwa kuidhinisha jumla ya Shl. 19,988,300,000.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
0 comments:
Post a Comment