TAASISI
zinazojihusisha na utetezi wa haki za binadamu, wanawake na watoto,
zimelaani kitendo cha walezi wa mtoto Nasra Rashid (4) kumficha katika
boksi tangu akiwa na miezi tisa hadi sasa na kutaka serikali ichukue
sheria haraka kwa wote waliohusika.
Taarifa
za mtoto Nasra kufichwa katika boksi kwa kipindi chote mkoani Morogoro
ziliibuliwa juzi na wasamaria wema baada ya kupewa taarifa kuwa ndani ya
nyumba ya Mariam Said aliyehamia mwaka 2010 kuna mtoto amefichwa ndani
ya boksi.
Chama cha
Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimesema kitendo cha
kuficha mtoto katika boksi ni cha kikatili ambacho serikali inapaswa
kukishughulikia kwanza kwa kuangalia sheria zinazomlinda mtoto za mwaka
2009.
Akielezea
sheria hiyo, mratibu wa Kituo cha Usuluhishi cha Tamwa, Gladness Munuo,
alisema sheria inayomlinda mtoto ya mwaka 2009 Sura ya pili, kipengele
cha 5(1), 5 (2) na 13 pamoja na mambo mengine vinaelezea kwa undani haki
na ustawi wa mtoto na kumuelezea ni nani na mambo gani anapaswa
kufanyiwa.
Munuo
alisema ili haki iweze kutendeka, serikali inatakiwa kutumia sheria hiyo
na nyingine kwa kuwa inaelezea dhahiri kuwa mtoto mwenye umri wa chini
ya miaka 18 anapaswa kupewa haki na kutotengwa/kubaguliwa kwa rangi
yake, mwonekano, jinsia, itikadi, dini, kabila na kufanyiwa ukatili wa
aina yeyote.
Kutokana
na kitendo hicho, Tamwa inaitaka serikali kumpeleka mtoto huyo kwa
madaktari bingwa kwa ajili ya kufanyiwa vipimo na kutibiwa na pia
kumtunza katika vituo maalumu vya kulelea watoto yatima, ili aangaliwe
kwa karibu na kupewa lishe.
Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema baada ya kusikia taarifa
hiyo kimeanza kufuatilia kwa karibu namna mamlaka za serikali
zinavyolishughulikia kisheria suala la mtoto huyo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa LHRC, Dk. Helen Kijo-Bisimba, alisema kituo hicho
kitaangalia namna mamlaka za kiserikali ambazo ni Ustawi wa Jamii, Jeshi
la Polisi Morogoro na Mahakama zitakavyofanyia kazi suala hilo.
"Tunalaani
kitendo cha walezi wa mtoto Nasra kumficha katika boksi na kumnyima
haki zake... tunaiomba jamii iliyoguswa na tukio hili kujua na kuchukua
majukumu yao kama wazazi na walezi," alisema.
Shirika
la Maendeleo ya Wanawake Afrika (Wildaf) pia limelaani na kueleza kwamba
limeanza kufuatilia kisheria kitendo hicho, ili kupata ukweli.
Mkurugenzi
wa Wildaf nchini, Dk. Judith Odunga, alisema amemwagiza mwakilishi wa
kituo cha Morogoro ambako tukio hilo limetokea, Flora Masoyi aanze
kufuatilia tukio hilo.
Kwa
mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro (RPC), Leonard Paul,
jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa kujua ni kitu gani
kilichosababisha mtoto huyo kufichwa katika boksi na kuwahoji wazazi na
walezi wake.
CHANZO TANZANIA DAIMA
CHANZO TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment