Wednesday, 21 May 2014

WENYE VYETI FEKI WAKAANGWA BUNGENI


Dodoma. Wabunge juzi jioni walichachamaa wakitaka mawaziri na wabunge wanaohusishwa na vyeti feki kulithibitishia Bunge juu ya uhalali wa vyeti vyao. 
Suala hilo lilijitokeza wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha vifungu vya bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka 2014/15.
Wabunge hao walikuwa wakijadili hoja iliyotolewa na Mbunge wa Ole, Rajabu Mohamed Mbarouk (Cuf) aliyeitaka Serikali kueleza ni kwa nini Baraza la Mitihani ya Taifa (Necta) linashindwa kudhibiti vyeti feki. Alisema kuna mchezo mchafu unaoathiri mfumo wa elimu nchini na uchumi wa Taifa.
Alisema kuzagaa kwa vyeti hivyo kunaifanya hadhi ya Necta kushuka na kukosa imani hata katika jumuiya za kimataifa.
“Suala la vyeti feki ambalo Baraza la Mitihani la Taifa ndilo lenye dhamana na jukumu la kuhakikisha halitokei katika taifa limeonekana kama suala la kawaida,” alisema na kuongeza; “Vyeti feki ni vingi kiasi kwamba linasababisha kuajiriwa kwa watendaji ambao ni feki na mawaziri mizigo.”
Alisema kuzagaa kwa vyeti hivyo kunasababisha kupata makatibu wakuu na watendaji feki.
Mbarouk alisema hivi karibuni katika Chuo cha Polisi cha Moshi walirejeshwa wadahiliwa 122 kwa sababu ya kukutwa na vyeti feki.
Alihoji ni kwa nini Necta inashindwa kudhibiti vyeti hivyo.
Akitoa ufafanuzi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema Necta baada ya kugundua udanganyifu wa vyeti ilibadilisha namna ya kuchapa vyeti hivyo.
“Hivi sasa vyeti vinavyotolewa vina Serial number, jina la mhitimu katika cheti cha kuzaliwa na picha na kwamba siyo rahisi kughushi vyeti hivyo,” alisema.
Hata hivyo, Mbarouk alikataa ufafanuzi huo na kusema asilimia sita ya wanaoomba kazi nchini wana vyeti feki.
Alitaka kufahamu hatua zilizochukuliwa ikiwamo za kinidhamu katika kukabiliana na suala hilo.
 CHANZO MWANANCHI

0 comments: