Sunday, 18 May 2014

UVCCM MANYARA WAMVAA LIPUMBA


Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba

Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Manyara, limemtaka Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) Prof Ibrahim Lipumba kuwaomba radhi Watanzania kwa kuwaita wajumbe wa Bunge la Katiba, Intarahamwe.
Akisoma tamko la Baraza hilo mjini Babati juzi, Katibu wa UVCCM mkoani Manyara, Ezekiel Mollel alisema jamii imesikitishwa na kauli hiyo hivyo Prof Lipumba anatakiwa kuomba radhi kwa kutoa lugha hiyo kwa wabunge hao.
“Vijana wa Manyara wamesikitishwa na kauli hiyo ya Prof Lipumba kwa vile wao wanataka Serikali tatu, sisi tutaendelea kuunga mkono Serikali mbili kwani ndizo zilizotufikisha hapa tulipo na tutaendelea kuzihitaji hizo,” alisema Mollel.
Pia, alitaja azimio lingine lililotolewa na Baraza Kuu hilo la mkoa wa Manyara ni kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa hotuba yake aliyoitoa April 25 mwaka huu jijini Dar es salaam, wakati akipokea maandamano ya vijana wa CCM.
“Azimio letu la mwisho la Baraza kuu la UVCCM mkoa wa Manyara ni kuhakikisha tunafanya ziara katika kata zote za mkoa wa Manyara na pia kuongeza wanachama wapya wa jumuiya yetu na CCM,” alisema Mollel.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Manyara, Regina Ndege aliwateua wajumbe watatu wa Baraza hilo Mosses Komba, Lusia Sulle na Yusuph Shaushi, kuwa wajumbe wa kamati ya utekelezaji wa mkoa huo.
Ndege alisema vijana wa mkoa huo wanatakakiwa kusimama kidete ili kuhakikisha wanaisimamia CCM na kuendeleza ushindi kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwaka kesho.
“Vijana tuna nguvu kubwa ya kukipigania chama na kuwashawishi wananchi kwa kutangaza utekelezaji wa ilani ya CCM mwaka 2010 hadi 2015 hadi tupate ushindi wa asilimia 90 kwenye chaguzi zote tutakazoshiriki,” alisema Ndege.

0 comments: