WAZIRI wa Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia
Simba, jana alizuiwa na walinzi wa Bunge kuingia ukumbini kutokana na kuvalia
mavazi yanayokiuka kanuni zinazoliendesha Bunge.
Simba
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi
(UWT), alifika bungeni hapo jana akiwa amevalia sketi na shati la mikono mirefu
lenye rangi ya kijani na alama za CCM.
Vyombo
vya Habari vilimshuhudia Waziri Simba alizuiliwa kuingia bungeni kutokana na
vazi lake hilo lenye alama za chama.
Katika
kuonesha kuwa Waziri Simba alivalia sare hiyo kwa makusudi, wakati akiingia
alijifunika kwa mtandio ili shati hilo lisionekane, lakini walinzi walimshtukia
kupitia upande wa mgongoni ambako mtandio huo haukufunika vizuri.
Alipotafutwa
kuzungumzia tukio hilo, Waziri Simba alijibu kwa kifupi kwa njia ya ujumbe
mfupi wa simu (sms) akisema; “achana na mimi”.
Hatua
hiyo inakuja wiki chache tangu Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kudai kuwa
aliandikiwa ujumbe na baadhi ya wabunge wakihoji kama mavazi ya kombati
yanayovaliwa na wabunge wa CHADEMA hayakiuki kanuni.
Ndugai
katika kauli yake hiyo alisema ziko kombati za rangi mbili, nyeusi na kaki
zinazovaliwa bungeni, kwamba na wengine wanataka kuja na kombati za rangi ya
kijani.
Hata
hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe na Mkurugenzi wa Mawasiliano
na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika walipinga kauli ya Ndugai wakidai
anafanya porojo za kisiasa bungeni.
Walisema
kuwa kombati ni mavazi yanayoruhusiwa na kanuni za Bunge na kufafanua kuwa kwa
mujibu wa kanuni, vazi la wanaume linaloruhusiwa ni pamoja na suti za safari
zinazovaliwa na CHADEMA.
Kwa
mujibu wa kanuni ya 149 (3) (a) kwa wanawake na (b) kwa wanaume kuna aina za
mavazi yanayopaswa kuvaliwa bungeni.
Kanuni
hiyo inasomeka kuwa kutakuwa na vazi rasmi kwa wabunge (a) kwa wanawake;- (i)
Vazi lolote la heshima yaani ambalo si la kubana mwili, lisiloonesha maungo
ambayo kwa mila na desturi za Kitanzania hayapaswi kuoneshwa na ni refu kuvuka
magoti, (ii) gauni la kitenge au blauzi inayovaliwa na kitenge au sketi ya
rangi yoyote (iii) kilemba cha kadiri au mtandio (iv) suti ya kike; au (v) vazi
linalovaliwa wakati wa eda.
b)
Kwa wabunge wanaume;- (i) suti ya Kiafrika au safari ya mikono mirefu au mifupi
yenye ukosi au shingo ya mviringo na yenye fulana au bila fulana ndani, ya
rangi moja, isiyokuwa na nakshi, pamoja au bila baraghashia;
(ii)
Vazi la kimwambao yaani kanzu rasmi na nadhifu, koti, baraghashia na makubazi
au viatu; (iii) suti kamili ya kimagharibi ya rangi kadiri isiyomeremeta; (iv)
koti aina ya blazer na tai, pamoja na suruali yoyote ya heshima; au (v)
tarbushi na kilemba cha Singasinga, au kilemba chochote kinachovaliwa kwa
mujibu wa masharti ya imani au mila.
Utoro
bungeni
Katika
kile kinachoweza kutafsiriwa wabunge kutotilia maanani umuhimu wa kuhudhuria
vikao, mijadala mbalimbali ya hotuba za bajeti imekuwa ikiendelea huku idadi
ndogo ikionekana ndani ya ukumbi.
Uchunguzi
wa wiki kadhaa, umebaini kuwa wabunge wengi wanahudhuria kipindi cha maswali na
majibu asubuhi na baada ya hapo wanatoka nje kuendelea na shughuli zao binafsi
au vyama vyao.
CHANZO: TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment