Wednesday, 2 July 2014

KOCHA MBEYA CITY FC AHITAJI CHANGAMOTO MPYA BAADA YA KUPATA `NONDOZ` YA CAF



 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhlOC7m3kmSBnmfpQqwG94xB5pbfv-sBx0mIBSw06yo3geW7VAkr1HUdbo4u0bk-5sBXGg3PjeWTB4fXkoch-fYifB3LIL6-1JHcZpapeXqJNG8JfaiX4Wq0WblL4CrWyRtNKaHcHDhOA/s1600/mb.jpg
Juma Mwambusi (wa kwanza kushoto) akiwa na Maka Mwalwisyi (wa pili kushoto) kwenye moja ya mechi ya Mbeya City fc katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.



ALIYEKUWA kocha msaidizi wa Mbeya City fc, Maka Mwalwisyi amedhamiria kupata changamoto mpya katika kazi yake ya ukocha baada ya kuamua kuachana na klabu hiyo kutokana na  mkataba wake kumalizika.

Akizungumza na MTANDAO HUU, Maka amesisitiza kuwa mara baada ya mkataba wake wa miaka miwili kumalizika tangu mei 30, aliamua kuhudhuria kozi ya CAF ya leseni B, hivyo anaona kuna haja ya kuachana na kazi ya kuwa kocha msaidizi wa Juma Mwambusi.

“Baada ya mkataba wangu kumalizika kulikuwa na kozi ya leseni B ya CAF ambayo ilikuwa inaendelea jijini Dar es salaam, nimehudhuria ile kozi, mwisho wa siku nilipomaliza nikatafakari na kuona kwamba kidogo nahitaji changamoto baada ya kuwa na daraja B”. Alisema Maka.

“Na nahitaji kuwa na timu yangu ambayo itanipa changamoto kama mwalimu wa daraja B, kocha Mwambusi ana falsafa yake na mimi nina falsafa yangu, kwa hiyo nahitaji falsafa yangu ionekane na sio kuwa chini ya kocha Mwambusi”. Aliongeza Maka.

Maka aliyesaidiana na Mwambusi kuifikisha Mbeya City katika nafasi ya tatu msimu uliopita alifafanua kuwa  hana tatizo na kiongozi yeyote wala mtu yeyote yule bali ameamua mwenyewe kuondoka katika klabu hiyo kwani anataka kuonyesha falsafa yake.

kwa sasa mwalimu huyo mwenye daraja B hajapata klabu yoyote ya kuinoa hapa nchini na amesema imekuwa ngumu kupata timu kwani watu walikuwa wanajua bado yupo Mbeya city.

Maka ni muumini mkubwa wa soka la vijana na hata vijana wengi wanaocheza kikosi cha pili cha Mbeya City walitokea katika akademi yake ya FOYSA.
Mbali na kutoa wachezaji hao, pia alitoa wachezaji mbalimbali wanaocheza timu tofauti tofauti za ligi kuu soka Tanzania bara.
 
Na Frank Momanyi, Dar es salaam

Imechapishwa Julai 2, 2014, saa 3:45 alasiri
 

0 comments: