MWENYEKITI
wa Friends Of Simba (F.O.S.), Zacharia Hans Poppe amesema umoja wao ni
sawa na ukuta wa chuma, maana yake wapinzani wa Simba SC katika soka ya
Tanzania sasa wasitarajie mteremko kwa klabu hiyo.
Kwa miaka mitatu sasa Simba SC haijatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na pia haijashiriki michuano ya Afrika.
Lakini
baada ya kigogo wa F.O.S., Evans Elieza Aveva kuchaguliwa kuwa Rais wa
kwanza wa klabu hiyo Jumapili, Simba SC inatarajiwa kurejesha makali
yake.
|
Mwenyekiti wa F.O.S., Zacharia Hans Poppe amesema Simba SC sasa itacheza mpira |
Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Poppe amesema kwamba Friends Of Simba ni ukuta wa chuma.
“Lango
la Simba SC sasa liko salama, Friends Of Simba ni beki imara,
haipitiki, sawa na ukuta wa chuma, sasa tunakwenda kucheza mpira,
nawaomba wana Simba SC wote waliojitenga kwa sababu ya matokeo mabaya,
warudi uwanjani timu yao ikicheza, watafurahi,”amesema.
Poppe
amesema uongozi uliopita wa Alhaj Ismail Aden Rage haukuwa na
ushirikiano, uliwagawa wanachama na akiwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji
alijitahidi kumshauri Mwenyekiti wake, lakini hakusikilizwa.
“Nilitumia
muda wangu mwingi kumshauri Rage, lakini hakunisikiliza. Friends
tulikuwa tunachangishana fedha, nampelekea Rage akafanyie shughuli za
klabu. Baadaye yeye anakwenda kusema, ni fedha za klabu.
Wewe
unadhani waliotoa fedha zao watajisikiaje? Basi, Friends wakaanza
kujitenga na huo ndiyo ukawa mwanzo wa Simba SC kufanya vibaya, sababu
hamasa ilipotea na wachezaji wakatumbukiwa nyongo.
Mishahara
ikawa inachelewa, mfumo mzima wa malipo ya wachezaji ukawa haueleweki,
timu ikawa ipo ipo tu. Lakini sasa tuna uongozi ambao utasikiliza
ushauri na kuufanyia kazi. Uongozi ambao utaifanya Simba SC kuwa ya
wana Simba wote,”amesema Hans Poppe.
Poppe
amesema anafahamu kuna ushindani mkali hivi sasa katika Ligi Kuu kutoka
kwa mabingwa, Azam FC, wapinzani wao wa jadi, Yanga SC walioshika
nafasi ya pili na hata Mbeya City, waliomaliza nafasi ya tatu, lakini
wao (F.O.S.) watatumia uwezo na uzoefu wao kuicheza Ligi wamalize juu ya
timu zote hizo.
Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
0 comments:
Post a Comment