Mmoja wa wanakikundi wa Kikundi
cha Vijana cha Maamuzi, Bw. Juma Ismail Hassan (aliyevaa tshirt ya blue)
akifafanua jambo wakati wa mkutano wa kikundi hicho na Katibu Mkuu,
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bibi. Sihaba Nkinga
(hayupo pichani) alipotembelea kikundi hicho mwishoni mwa wiki Kilwa
Kivinje, Mkoni Lindi.Katibu Mkuu aliktembelea kikundi hicho ambacho kiko
kwenye hatua za kupunguza matumizi ya dawa za kulevya ili kukihamasisha
kuacha kabisa matumizi ya dawa hizo na badala yake wajikite katika
shughuli za uzalishaji.
Katibu Mkuu, Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Bibi. Sihaba Nkinga (wa pili kulia) akiwa
katika picha ya pamoja na Kikundi cha Maamuzi pamoja na baadhi ya
Viongozi wa Wilaya ya Kilwa. Wa tatu kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa
Maendeleo ya Vijana, Bw. James Kajugusi, anayefuata ni Kaimu Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Bw. Charles Mwaitege na wa kwanza
kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilwa, Bw. Simon Manjurungu na wa
kwanza kulia ni Afisa Utamaduni wa Mkoa wa Lindi, Bibi Makalaghe
Shekalaghe Nkinda.
Katibu wa Kikundi cha Sayari,
Bibi. Mwanaisha Ali akikabidhi Risala ya Kikundi hicho kwa Katibu Mkuu,
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bibi. Sihaba Nkinga
mwishoni mwa wiki alipotembelea kikundi hicho kwa ajili ya kukagua
maendeleo ya shughuli za vikundi vya Vijana Wilayani Kilwa, Mkoani
Lindi.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Sayari,
Bw. Ramadhan Sungura akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Bibi. Sihaba Nkinga (hayupo pichani)
wakati alipokutana na kikundi hicho kwa ajili ya kukagua maendelo ya
shughuli za kikundi hicho mwishoni mwa wiki.
…………………………………………………………
(Na Concilia Niyibitanga)
Halmashauri zote nchini zinawajibika kutenga maeneo kwa ajili ya
shughuli za maendeleo ya vijana pamoja na kuwatengea vijana asilimia 5
ya mapato ya halmashauri husika kwa ajili ya kuwezesha shughuli hizo.
Hayo yamesemwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Bibi Sihaba Nkinga wakati akikagua maendeleo ya
vijana Wilayani Kilwa, mkoani Lindi.
Amesema kuwa vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa na kwa maana hiyo
wanatakiwa waongozwe na wawezeshwe ili kushiriki kikamilifu katika
shughuli za maendeleo kwa lengo la kujikwamua katika umaskini.
Vijana wanatakiwa kuhamasishwa kuunda na kujiunga katika vikundi
vya uzalishaji mali na kuunda SACCOS za vijana ili waweze kupatiwa
mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa ajili ya kuongeza mitaji
na kupanua uzalishaji. Amesema Bibi Nkinga.
Akiongea na Kikundi cha Vijana cha Maamuzi kilichopo Kilwa
Kivinje ambacho kina wanachama 21 ambao hapo awali wamekuwa
wakijihusisha na matumizi ya madawa ya kulevya na sasa kuamua kupunguza
matumizi ya madawa hayo, aliwataka kuendelea kupunguza na hatimaye
kuacha kabisa kwani madawa hayo yanaathiri afya zao na kupunguza uwezo
wa uzalishaji.
Aidha, alikitaka kikundi hicho kuendelea kuwahamasisha vijana
wenzao walioathirika na madawa hayo kujiunga katika kikundi hicho
ikizingatiwa kuwa Wilaya ya Kilwa ina Vijana zaidi ya 100 walioathirika
na matumizi ya madawa ya kulevya.
Aliwataka kuendelea kushiriki katika shughuli za kujitolea
wanaozifanya sasa za usafi wa mazingira na wasikate tamaa wasonge mbele
kwa kuwa familia zao na jamii nzima inawategemea wao kama nguvu kazi ya
taifa.
Wakati huo huo, akiongea na kikundi cha vijana cha Sayari chenye
wanachama 22 kinachojihusisha na biashara ya uuzaji chakula cha mifugo
aliwataka kuendelea kuwa wabunifu na kuanzisha miradi mingi zaidi ya
kuwaingizia kipato na kutunisha mfuko wao.
Pia aliwataka kuhakikisha kuwa wanasajili kikundi chao ili
kiweze kutambulika kisheria na pia wajiunge katika SACCOS ya vijana ili
iwe rahisi kupatiwa mikopo ya kuendeleza shughuli zao za uzalishaji
mali.
0 comments:
Post a Comment