
HOTUBA YA MHESHIMIWA WAZIRI WA FEDHA, SAADA MKUYA SALUM (MB)
AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA FEDHA KWA
MWAKA 2014/15
UTANGULIZI:
1.
Mheshimiwa Spika, kufuatia
taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, naomba kutoa hoja kwamba Bunge
lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na
Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2014/15.
2.
Mheshimiwa Spika,
awali
ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa
kuniwezesha kuwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya mwaka 2014/15. Aidha,
natoa shukrani zangu za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Ninaahidi kwamba
nitatekeleza jukumu hili kwa weledi na uadilifu. Vile vile, nawapongeza Mhe.
Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Mhe. Adam Kighoma Ali Malima (Mb) kwa kuteuliwa
kuwa Naibu Mawaziri wa Wizara ya Fedha. Kadhalika, namshukuru pia aliyekuwa
Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Janeth Zebedayo Mbene (Mb) kwa utendaji kazi wake
mahiri na tunamuombea Mwenyezi
Mungu ampe nguvu na afya njema katika kazi zake mpya Wizara ya Viwanda na
Biashara. Nichukue pia fursa hii kumpongeza Bw. Rished M. Bade kwa kuteuliwa
kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania.
3.
Mheshimiwa Spika, napenda
kukupongeza wewe mwenyewe, Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa
Bunge kwa kuongoza vyema majadiliano ya Bunge la Bajeti.
4.
Mheshimiwa Spika, naomba
nitumie nafasi hii kuishukuru kwa namna ya pekee Kamati ya Kudumu
ya Uchumi, Viwanda na Biashara chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Luhaga Joelson
Mpina (Mbunge wa Kisesa) na Makamu wake Mhe. Dunstan Luka Kitandula (Mbunge wa
Mkinga) kwa maoni, ushauri na mapendekezo waliyoyatoa kwa Wizara wakati wa
kuchambua mapendekezo ya Bajeti ya Wizara ya Fedha. Aidha, nachukua nafasi hii
kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti Mhe. Andrew John Chenge
(Mbunge wa Bariadi Magharibi) pamoja na Kamati nzima kwa ushauri wao. Katika
uandaaji wa hotuba hii, Wizara imezingatia ushauri na mapendekezo ya Kamati
hizo pamoja na ushauri na maoni ya hoja mbalimbali zilizotolewa wakati wa mjadala wa bajeti
ya Wizara kwa mwaka 2013/14.
5.
Mheshimiwa Spika, kama
unavyofahamu, Wizara ilipata pigo kwa kuondokewa na kiongozi wetu
mkuu Marehemu Dkt. William Augustao Mgimwa. Tunawashukuru Viongozi wa Serikali,
Waheshimiwa Wabunge, Washirika wa Maendeleo, Taasisi mbalimbali pamoja na
wananchi kwa ushirikiano waliotupa kipindi chote cha msiba. Tumeendelea kuenzi
misingi imara aliyotujengea marehemu katika kutekeleza majukumu ya Wizara.
Aidha, tunapenda kutoa pole kwa ndugu na jamaa kufuatia kifo cha aliyekuwa
Mbunge wa Chalinze Marehemu Saidi Ramadhani Bwanamdogo. Vile vile, napenda
kutoa pole kwa Mheshimiwa Zuberi Zitto Kabwe kwa msiba wa mama yake mzazi
aliyefariki tarehe 01 mwezi Juni, 2014. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu
mahali pema peponi. Amina.
6.
Mheshimiwa Spika, tarehe
27 mwezi Mei 2014, Wizara ya Fedha ilipata pigo tena baada ya
kifo cha mke wa Katibu Mkuu - Hazina. Kwa namna ya kipekee naomba nitumie tena
fursa hii kutoa pole kwa Dkt. Servacius Likwelile kwa kufiwa na mkewe.
Hata hivyo Dr. Likwelile ameendelea kutekeleza majukumu yake katika kipindi
chote cha msiba.Wizara inatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa familia yake
kwa msiba wa mpendwa wao. Namuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho ya marehemu
mahali pema peponi. Amina.
7.
Mheshimiwa Spika, napenda
kuwapongeza, Mhe. Yusuf Salim Hussein Mbunge wa Chambani, Mhe.
Godfrey William Mgimwa (Mbunge wa Kalenga) na Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete
(Mbunge wa Chalinze) kwa kuchaguliwa kwao.
0 comments:
Post a Comment