Hassan Mtenga, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa |
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Manispaa ya
Iringa kimeingia katika vuta nikuvute na baraza la madiwani la halmashauri hiyo
kikipinga ziara ya madiwani wake kufanya ziara ya mafunzo katika mikoa ya Dar
es Salaam, Lindi na Mtwara.
Katika kupinga ziara hiyo CCM
imemuandikia barua Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba ikieleza sababu
zake za kufanya hivyo; barua hiyo imefikishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk
Christine Ishengoma.
Katibu wa CCM wa manispaa hiyo, Hassan
Mtenga ambaye pia ni Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa alisema; “chama hakioni
kama ziara hiyo inataja kwasasa.”
Mtenga alisema wananchi wa manispaa ya
Iringa wanakabiliwa na kero nyingi ikiwemo ya ubovu wa miundombinu ya barabara
zake zilizoharibiwa na mvua zilizopita za masika.
“Mamilioni ya fedha wanayotaka kuyatumia
kwenye ziara hiyo yanaweza kusaidia kurekebisha miundombinu hiyo na mambo
mengine muhimu kwa wananchi wa manispaa yetu,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Ishengoma ambaye
kiutaraibu ndiye mwenye dhamana ya mwisho ya kukubali au kukataa ziara hiyo alisema
ameanza kulishughulikia suala hilo.
“Nimekutana na Katibu wa CCM, Meya na
Mkurugenzi wa Manispaa; katika ushauri wangu wa awali nimeelezea umuhimu wa
ziara hiyo, hata hivyo nimeshauri ifanyike katika mkoa mmoja wa Dar es Salaam
kama ikibidi,” alisema.
Alisema halmashauri hiyo inaweza kuokoa
fedha nyingi kwa kuachana na ziara ya Lindi na Mtwara na kuzitumia fedha
zitakazookolewa kwa shughuli zingine za maendeleo.
Awali Mstahiki Meya wa Manispaa ya
Iringa, Amani Mwamwindi alisema wataupokea ushauri wowote utakaotolewa na mkuu
wa mkoa kuhusiana na ziara hiyo.
“Tutasikia ushauri wa mkuu wa mkoa,
lakini na wa chama pia kwasababu sote tunatekeleza Ilani ya CCM; tutaona suala
hili limekaaje baada ya kufikishwa mezani na tutakuja na maamuzi ya mwisho,”
alisema.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa,
Theresia Mahongo alisema bajeti kwa ajili ya ziara hiyo (hakutaja kiasi chake)
ilipitishwa mwaka jana.
Alisema madiwani hao walitaka kwenda
Lindi, Mtwara na Dar es Salaam kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali
yanayoweza kusaidia kuharakisha maendeleo ya manispaa ya Iringa.
Alisema wakati ziara ya Lindi inalenga
kujifunza mbinu mpya za kuhamasisha utalii, ile ya Mtwara inalenga kujifunza miradi
ya ujenzi wa majengo bora na ya Ilala Dar es Salaam mbinu za ukusanyaji mapato.
Alisema kufanyika kwa ziara hiyo
kutategemea maelekezo yatakayotolewa na Mkuu wa mkoa na meya wa manispaa hiyo
kwa mujibu wa taratibu za kiutendaji.
Pamoja na ufafanuzi wa watendaji hao,
madiwani wa manispaa hiyo wameganyika kuhusiana na ziara hiyo, huku wachache
wakiunga mkono ushauri wa CCM na wengine wakitaka ifanyike.
Baadhi ya madiwani wa CCM ambao ni wengi
katika baraza hilo (hawakutaka majina yao yatajwe) walisema wanaunga mkono
uamuzi wa CCM wa kupinga ziara hiyo.
Mmoja wa madiwani hao alisema pamoja na umuhimu wa ziara hiyo, fedha
hizo zinaweza kufanya makubwa kwa maendeleo ya manispaa hiyo.
“Na tungependa kwa lolote litakalofanywa
itangazwe wazi kwamba limetokana na fedha zilizokuwa zilipwe kwa madiwani; hiyo
itatupa heshima kubwa na hasa kwa kuzingatia kwamba tunakaribia kufanya
Uchaguzi Mkuu,” alisema.
Diwani mwingine alisema ziara hiyo haina
maana sana kwao kwa kuzingatia kwamba wana muda mfupi kabla ya kuingia katika
harakati za Uchaguzi Mkuu ujao.
“Tunaweza kwenda ziarani, lakini lini
hicho tutakachojifunza tutahakikisha kinatekelezwa; sioni haja ya kwenda ziara
hiyo,” alisema.
0 comments:
Post a Comment