ASASI ya Tanzania Horticulture
Associatino(TAHA)yenye makao makuu mkoani Arusha imetoa mafunzo kwa wakulima wa
mazao ya Kabeji kutoka vijiji 12 vya Wilaya ya Mbeya yaliyofanyika kwa vitendo
katika mashamba darasa yaliyopo Simambwe kata ya Tembela wilaya ya Mbeya mkoani
hapa.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha
mafunzo hayo, Afisa Ufundi kutoka TAHA, Isaack Ndamanyile, alisema lengo la
kutoa mafunzo hayo ni kutoa teknolojia bora za kisasa kwa wakulima na kutumia
mbolea na madawa.
Alisema mafunzo hayo hadi sasa
yamewanufaisha wakulima kutoka vikundi 12 kati ya 35 ambavyo vimeshiriki
mafunzo hayo moja kwa moja ambapo wamejifunza jinsi ya kuandaa mashamba
matumizi ya mbolea na mbegu bora za mazao ya kabeji.
Alisema mbali na mafunzo hayo wakulima
pia watatafutiwa masoko ya mazao yao ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha na
wafanyabiashara wakubwa wa kununua mazao yao.
Aliongeza kuwa wakulima wamefundishwa
kulima mazao hayo kutokana na kutoa matunda baada ya muda mfupi hivyo
kumnufaisha mkulima moja kwa moja badala ya kusubiri muda mrefu.
Alitoa mfano wa zao la kabeji kuwa
linavunwa baada ya miezi mitatu baada ya kupandwa hivyo mkulima anakuwa na
uhakika wa kupata mavuno kwa muda mfupi baada ya kulima kwa kuzingatia kanuni
na ushauri wa kitaalamu.
Baadhi ya wakulima waliofika katika
mafunzo hayo walisifia Asasi hiyo kwa hatua yao ya kuwafikia wakulima na kutoa
mafunzo katika mashamba yao na kwamba hilo litasaidia kuwainua kiuchumi.
Aidha walisema baada ya kulima kwa
kuzingatia ushauri wa kitaalamu wameanza kusumbuliwa na wanunuzi mashambani
kabla ya mazao kukomaa kutokana na mwonekano ulivyo.
Walisema jinsi walivyofundishwa kilimo
cha kisasa mkulima anao uwezo wa kujua thamani ya mazao yake hata kabla ya
kuvuna kutokana na mpangilio uliowekwa ambao utaondokana na kudhurumiwa na
wachuuzi wa mazao mashambani.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
0 comments:
Post a Comment