Monday 3 June 2013

MWILI WA MAREHUMU WA KAA MOCHWARI MIAKA 10 SASA

Kenya — Mwili wa mwanamke mmoja umesalia katika mochwari moja ya kibinafsi kaunti ya Machakos kwa miaka kumi kutokana na wanawe na ndugu zao wa kambo wakizozania ardhi ya baba yao huku bili ya kuhifadhi mwili huo katika ufuo huo inakaribia kugonga fedha za Kenya, shilingi milioni mbili.

Wasimamizi wa Machakos Funeral Home mjini Machakos, Jumapili walithibitisha kwamba mwili wa Esther Nzakwa Kitivo, uko katika chumba hicho tangu 2004.

Watoto wa kambo wa Nzakwa aliyekufa Agosti 31, 2004, walikataa mwili huo kuzikwa karibu na kaburi la mumewe katika kipande cha ardhi eneo la  Kitanga, Kalama, Machakos. Walienda mahakamani na kupata agizo la kumzuia mwana wa marehemu, Bw Michael Musau Kitivo, kumzika mama yake katika ardhi hiyo wakidai baba yao, marehemu Gideon Kitivo Ndambuki aliikabidhi kwa Maurice Ndambuki Kitivo, mwana wa mke mwenza wa marehemu Nzakwa.

Katika kesi aliyowasilisha mbele ya mahakama ya Machakos mwaka 2004, iliyopelekea kusimamishwa kwa 
mazishi ya Nzakwa hadi wakati huu, Ndambuki alidai mwili wa mama yake wa kambo haungezikwa kwenye ardhi hiyo kwa sababu ilikuwa yake aliyopata kutoka kwa baba yake kabla ya kuaga dunia.

Alimtaka Musau, amzike mama yake katika ardhi aliyogawiwa na baba yao, lakini Musau akasisitiza kwamba sharti mama yake azikwe kando ya kaburi la mumewe. Alisema kulingana na mila za jamii ya Wakamba, sharti mke wa kwanza azikwe kando ya mumewe.

Lakini mahakama ilikubaliana na Bw Ndambuki na kupuuza madai ya Musau na kusimamisha mazishi.

“Ukoo wa marehemu ulikuwa umeamua eneo la kumzika marehemu, na  mahakama haiwezi kutoa uamuzi mwingine,” akasema aliyekuwa Hakimu Mkazi wa Machakos T. O Okello kwenye uamuzi wake.

Lakini mzozo huo haukukomea hapo na Musau, anayedai anapasa kusimamia mali ya baba yake, akaamua kukata rufaa katika mahakama kuu.

Hata hivyo mahakama kuu iliidhinisha uamuzi wa hakimu kwamba ardhi aliyotaka kumzika mama yake ilikuwa ya nduguye wa kambo, Ndambuki.

“Nguvu nyingi zimeharibiwa kuhusu ufafanuzi wa mila za Wakamba na kwa maoni yangu hayo sio masuala halisi yanayohusu kesi hii,” akasema Jaji Sitati aliyesikiliza rufaa hiyo.

Akipuuza rufaa hiyo, jaji alisema Musau hangeweza kumzika mama yake kwa nguvu katika ardhi hiyo kwa sababu hakuna sheria za jamii ya Wakamba zinazosema mke azikwe kando ya mumewe.

Musau alisema baada ya uamuzi huo wa mahakama ya rufaa, aliwasilisha kesi akitaka mahakama iamue mrithi wa ardhi hiyo anayoshikilia kwamba ilikuwa ya babake na hakumpatia Bw Ndambuki.

Kesi hiyo inaendelea na itatajwa Julai 18 mwaka huu.


Kwa msaada  SwahiliHub

0 comments: