Monday 3 June 2013

LINDI NA M MTWARA WAPITISHA MAZIMIO 8

Zaidi ya Wananchi 976 kutoka katika mikoa ya Lindi na Mtwara wameitaka serikali iwaombe radhi kwa madai kwamba, imepotosha hoja yao ya msingi kuhusu gesi na hivyo kuwachonganisha na Watanzania wenzao wa mikoa mingine nchini.

Wamesema hoja yao ya msingi iliyopotoshwa ni ya kutaka kuhakikishiwa gesi iliyogunduliwa mkoani Mtwara, inawanufaisha, na hawajawahi kudai isipelekwe katika mikoa mingine nchini.

Hiyo ni miongoni mwa maazimio manane yaliyopitishwa na wananchi wa mikoa hiyo katika kongamano lao lililofanyika katika viwanja vya ofisi za Chama cha Wananchi (CUF), jijini Dar es Salaam jana, ambao 
walichanga Shilingi 352,350/= kwa ajili ya mfuko maalum wa kuwasaidia watu waliokamatwa kufuatia vurugu zilizotokea mkoani Mtwara kuhusiana na gesi.

Kongamano hilo lililohutubiwa na Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, liliandaliwa maalumu kwa ajili ya wananchi wa mikoa hiyo kujadili gesi.

Akisoma maazimio hayo kwa niaba ya wananchi, Abdulrahman Lugone, alisema wataendeleza makongamano mengine zaidi katika maeneo tofauti nchini ili kueneza taarifa nzuri kuhusu gesi zilizowasilishwa na Profesa Lipumba katika kongamano la jana. Aliyataja maazimio mengine kuwa ni pamoja na:
  • Wanamtaka Rais Jakaya Kikwete kumwajibisha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, kutokana na nguvu kubwa iliyotumika kudhibiti vurugu za Mtwara na kusababisha vifo vya wananchi, akiwamo mjamzito asiyekuwa na hatia.
  • Kutekeleza matakwa yao, kuanzisha kamati ya watu wa mikoa ya kusini na kuanzisha pia mfuko wa kuchangia gharama za wakili atakayewateteta watu waliokamatwa kufuatia vurugu hizo.
  • Iwapo gesi ya Songosongo haiwanufaishi wananchi wa Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, basi gesi ya Mtwara isitoke mpaka ‘kieleweke’.
  • Wananchi wa mikoa ya kusini wamebaini kuwa serikali haiwatakii mema na haiwataki, hivyo kwa pamoja watatumia fursa ya chaguzi zijazo kuinyima CCM nafasi za uongozi; kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, mitaa, udiwani, ubunge hadi urais. 
  • Azimio lingine wamekubaliana kufanya maandamano makubwa ya kitaifa ili kufikisha ujumbe ulio sahihi.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro, alisema maandamano hayo yatafanyika Juni 29, mwaka huu, na yataanzia eneo la Buguruni Sheli hadi Ikulu.

Profesa Lipumba, katika hotuba yake alisisitiza haja ya nchi kuwa na umoja wa kitaifa na kwamba chanzo cha mgogoro wa gesi ni serikali kushindwa kutekeleza ahadi zake kwa wananchi wa Mtwara na kusema watahakikisha maandamano hayo yanafuata taratibu zote za kisheria.

---
via NIPASHE
 

0 comments: