Waunga mkono kauli ya Waziri wa Nishati na Madini
• Wataka wenye uwezo kuacha ubinafsi na ubepari
• Wataka raslimali za madini ziwanufaishe Watanzania wote
Na. Issa Mtuwa – STAMICO
Wananchi wameiomba serikali kuhakikisha rasilimali za Madini
zinawanufahisha Watanzania wote na sio wachache wenye uwezo. Kauli
ambayo imewahi kutolewa siku za hivi karibuni na Waziri wa Nishati na
Madini Prof. Sospeter Muhongo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati walipotembelea katika
banda la Shirika la Madini la Taifa STAMICO katika maonesho ya 38 ya
Biashara ya Kimataifa (SABASABA) 2014, wananchi hao wamesema ili azma
hiyo iweze kutimia ni vyema Serikali ikaijenga uwezo STAMICO kifedha na
vitendea kazi ili iweze kutekeleza miradi ya uchorongaji na uchimbaji
madini itakayowanufaisha wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake alioambatana nao katika banda
la STAMICO, Mkazi wa mkoa wa Mara, Bw. Joel M. Changarawe amesema katika
kujenga uwezo wa kifedha wa Shirika hilo, Serikali haina budi
kuendeleza azma yake ya kuikabidhi STAMICO migodi yote mikubwa ya Madini
iweze kumiliki kwa niaba ya Watanzania na kuzalisha ili kuongeza tija
kwa Taifa.
Jacqueline Aisaa akitoa maoni yake
kuhusu sekta ya Madini wakati wa maonesho ya 38 ya Biashara ya
Kimataifa Sabasaba 2014. Anae msikiliza ni Bw. Issa Mtuwa Afisa Uhusiano
wa STAMICO.
“Nashauri Watanzania tuache ubinafsi na ubepari. Naishauri
serikali Migodi yote ya Madini yenye RESERVE (akiba) kubwa imilikiwe na
STAMICO kwa niaba ya Watanzania badala ya kukabidhi kwa Watanzania
wachache wenye tamaa ya utajiri ambao wanamiliki vitalu vya madini
kupitia migongo ya kampuni za kigeni” alisema Bwana Joel kwa kuandika
kwenye kitabu maalum cha Maoni, ushauri na kero za Wananchi.
Naye Jacqueline Aisaa mkazi wa Masama-Moshi, ambaye pia ni
mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Shahada ya kwanza katika Chuo cha
usimamizi wa fedha (IFM) alisema serikali iipe meno STAMICO ya usimamizi
wa hisa zote za serikali kwenye migodi yote na usimamizi wa jumla
katika sekta ya Madini ili Wananchi waweze kunufaika na raslimali hizo.
0 comments:
Post a Comment