SHIRIKA
la Madini la Taifa (STAMICO) leo linafunga upokeaji wa maombi ya nia
(expression of interest) ya makampuni yanayotaka kuingia ubia na STAMICO
katika uendelezaji wa mradi uchimbaji makaa ya mawe na ufuaji umeme
huko Kiwira.
STAMICO ilitangaza mwezi uliopita kukaribisha maombi hayo
yatakayowezesha ubia huo kupata fedha za kughramia mradi kwa asilimia
100 na kushiriki kuendesha mradi huo.
Makampuni yenye nia ya kuwekeza kwa ubia na STAMICO yalitakiwa
kuwasilisha maelezo ya kutosha kuhusu makampuni hayo pamoja na
uthibitisho wa uzoefu wa kuendesha migodi ya makaa ya mawe na ufuaji
umeme kwa kutumia makaa ya mawe.
Makampuni hayo pia yanatakiwa kuonesha uzoefu wao katika
kuendesha miradi kama hiyo sehemu nyingine Duniani ikiwemo nchi za
Afrika.
Aidha STAMICO inayataka makampuni yenye nia kuonesha uwezo wake wa kifedha na kiufundi.
Maombi ya makampuni hayo pia yanatakiwa kuonesha namna gani
yatakavyotumia utaalamu na huduma za ndani kama ilivyoainishwa kwenye
Sheria ya Madini ya mwaka 2010.
Makampuni ambayo maombi yake yatakubaliwa na STAMICO
yatakaribishwa kuchukua nyaraka za zabuni na kuwasilisha michanganuo yao
ya kiufundi na kifedha.
Uendelezaji wa mradi Kiwira umegawanyika katika sehemu nne
ambazo ni upanuzi wa mgodi uliopo wa chini ya ardhi, ujenzi wa mgodi wa
wazi, ununuzi na ufungaji wa mitambo ya kufua umeme na ujenzi wa njia za
kusafirisha umeme.
Upanuzi wa mgodi wa chini utakaoongeza uzalishaji wa makaa ya
mawe kutoka tani 150,000 kwa mwaka hadi tani 300,000 kwa mwaka wakati
mgodi mpya wa wazi unategemea kuzalisha tani milioni 1.2 za makaa ya
mawe kwa mwaka.
Uendelezaji wa mradi huu pia utahusisha ujenzi wa mtambo wa
kufua umeme wa Megawati 200 na ujenzi wa njia ya kusafirisha yenye urefu
wa km 100 toka eneo la Kiwira Wilayani Ileje hadi Mbeya mjini.
Ujenzi wa mgodi wa Kiwira ulianza mwaka 1983 na kukamilika 1988
kwa gharama za Sh.4.29 bilioni, ukiwa ni mkopo wa masharti nafuu kutoka
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Mwezi Juni, 2005 mgodi wa Kiwira ulibinafsishwa kwa kampuni ya
Tan Power Resources (TPR) kwa asilimia 70 na Serikali ilibaki na
asilimia 30.
Ubia huu ulilenga zaidi katika kuzalisha umeme wa MW 200 kwa kutumia makaa ya mawe ifikapo 2009.
Katika kipindi cha kuanzia Juni, 2005 hadi Julai,2009
zilifanyika kazi mbalimbali za kuendeleza mgodi huu. Miongoni mwa kazi
hizo ni upembuzi yakinifu na usanifu wa mgodi, upembuzi yakinifu kwa
ajili ya kufua umeme wa MW 200 na kusainiwa kwa mkataba wa mauzo ya
umeme wa MW 200 na TANESCO mnamo mwezi Agosti 2006.
Kazi nyingine ni kusainiwa kwa mikataba ya ujenzi na
utengenezaji wa mitambo, kukamilika kwa tathmini nne za mazingira na
kukamilika kwa upimaji wa njia ya umeme ya kV 220 kutoka eneo la mgodi
kwenda Mbeya.
Mwezi Julai,2009 Serikali iliamua kuurudisha mgodi wa Kiwira
Serikalini kwa asilimia 100 kutokana na kukwama kwa uendelezaji wa Mgodi
chini ya TPR na kushindwa kuwalipa wafanyakazi mishahara yao kwa muda
mrefu tangu mwezi Agosti,2008.
Baada ya majadiliano ya muda mrefu, tarehe 28, Novemba 2011
Serikali na TPR zilifikia muafaka wa Serikali kuuchukua mgodi kwa
asilimia 100.
Mtaji unaohitajika kuendeleza mgodi huu ni takriban Dola za
Marekani Milioni 400 ambazo zinaweza kupatikana kwa njia mbili;kwa
kumtafuta mbia mwenye uwezo wa fedha au kwa kukopa katika taasisi
mbalimbali za fedha.
Aidha STAMICO inaangalia uwezekano wa kufanyia ukarabati mashine
ya kufua umeme ya MW 6 iliyopo katika mgodi huu ili umeme
utakaozalishwa uuzwe TANESCO.
Katika mwaka wa fedha 2014/15, Serikali imeitengea STAMICO Shs.
bilioni 5 kwa ajili ya usimamizi na uangalizi wa mgodi katika kipindi
hiki cha mpito.
Friday, 18 July 2014
HOME »
» Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lafunga upokeaji wa maombi ya nia (expression of interest)
0 comments:
Post a Comment