Wakazi wa Kitongoji cha Bondeni,
Kijiji cha Ngurdoto, Kata ya Maji ya chai, Wilayani Arumeru Mkoani
Arusha, wameiomba Serikali kuwachukulia hatua kundi la zaidi ya watu 30
wanaofanya uhalifu wa wizi wa kukaba na kubaka.
Kundi hilo la vijana kutoka Tengeru
na Sing’isi wilayani humo, ambalo ni hatari kama makundi ya mbwa mwitu
na panya rodi, huvamia majumbani kwa watu saa 7 hadi saa 9 usiku na
kupora vitu ikiwemo fedha, tv na redio.
Wakizungumza na waandishi wa habari
juzi, baadhi ya wakazi wa eneo hilo ambao waliogoma kutaja majina yao,
walidai kuwa kundi hilo linafanya uhalifu kwenye nyumba ambazo hazina
wanaume na kuwabaka wanawake.
Walidai kuwa mara nyingi, ikifika
wakati wa usiku watu hushindwa kutembea kwa hofu ya kukutana na kundi
hilo kwani baadhi yao ambao inadaiwa kuwa wana maambukizi ya virusi vya
ukimwi hubaka wanawake wa kitongoji hicho.
“Tunaiomba Serikali ichukue hatua,
kwani ni juzi tu hapa walivamiana nyumbani kwangu na waliua mbwa wangu
baada ya kuiba redio, tv na fedha taslimu sh1 milioni,” alisema mmoja
kati ya waathirika wa kitongoji hicho.
Walisema hivi sasa wanaishi kwa hofu
kwani awali kulikuwa na kikundi cha polisi jamii na ulinzi shirikishi na
hayo matukio hayakuwepo na Serikali haijachukua hatua au kukemea hali
hiyo ambayo haipo kwenye vijiji vingine.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa kitongoji
cha Bondeni Richard Shirima alisema awali kikundi hicho kilikuwa
kinasumbua eneo hilo ila hivi sasa hali ni shwari kwani waliweza
kuwathibiti vijana wote wanaofanya uhalifu katika kitongoji hicho.
“Kama watakuwa wanafanya matukio hivi
sasa hao watakuwa wanakuja upya kwani hiyo hali tulishaithibiti ila
tutazifanyia kazi hizi taarifa zako ulizotupatia na kuhakikisha hali ya
amani inazidi kuwepo eneo hili,” alisema Shirima.
Na Gladness Mushi, Arusha
0 comments:
Post a Comment