Hakika
cheo ni dhamana, hivyo ni muhimu kwa wenye dhamana hiyo kujitambua na
kuonyesha wanavyoweza kubeba dhamana hiyo kwa jamii husika.
Halima Dendegu, ambaye sasa ni Mkuu wa
Wilaya ya Tanga, mkoani Tanga anaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa
kuonyesha alivyobeba dhamana hiyo ya kuiongoza wilaya kutokana na
kugeukia kundi la vijana wilayani kwake akidhamiria kuwakomboa.Dendegu aliyeteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, Mei mwaka 2012 kuwa mkuu wa wilaya hiyo anaeleza kuwa baada ya kuingia wilayani humo alifanya utafiti na kubaini kundi kubwa la vijana likijihusisha na matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu mbalimbali.
"Nilianza kubaini vijiwe vingi vya vijana na hawana ajira, nilipofuatilia zaidi niligundua wengi wametumbukia katika matumizi ya dawa za kulevya,"anasema Dendegu na kuongeza
Anabainisha kuwa baada ya kuwahoji vijana hao walitoa sababu mbalimbali za kujiingiza kwenye dawa za kulevya ikiwamo kukosa ajira, makundi na kukata tama.
"Wengine walisema walishawishiwa, wapo waliosema kiingiacho mjini siyo haramu, waliokuwa wakiuza dawa hizo, hata walioshindwa kutimiza malengo yao maishani," anasema Dendegu.
Anaongeza: "Kwa sababu hiyo, nimeanzisha kituo ili kuwatibu, kimeanza na vijana 150 na 78 kati yao wameanza matibabu wakiwamo wasichana 28."
Anabainisha kwamba kwa kuwa lengo lake ni kuwaepusha wasirudi kwenye dawa za kulevya katika kituo hicho ameanzisha pia utoaji elimu ya ujasiriamali.
"Tayari tumebabini wenye vipaji mbalimbali, wapo wapenda mpira wa miguu, watengenezaji sabuni hata wasanii wa muziki wa kizazi kipya."
Anasema kuwa ili kuwajenga zaidi kiafya na kuanikiza vipaji vyao, kila Jumamosi huandaliwa bonanza linaloendana na michezo mbalimbali.
"Pia nimeanzisha michuano ya mpira 'Dendegu Cup' litazinduliwa Juni mwaka huu ili kuibua vipaji zaidi, naamini tutatoa vijana wa kucheza timu kubwa,"anasema akidokeza kuwa hata yeye anapenda na kucheza mpira wa pete, volleyball, pia kuimba
Anasema kuwa katika tamasha hilo la uzinduzi vijana watafundishwa stadi za maisha na kupewa fursa za mikopo ili kuwainua kiuchumi.
Anabainisha kuwa baadhi ya vijana hao tayari wameunda kikundi cha muziki wa kizazi kipya, ambalo lilitoa burudani wakati wa ziara ya Rais Jakaya Kikwete Machi 27, pamoja na sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Aprili 26, jijini Dar es Salaam.
"Lengo langu ni kuwawezesha hawa vijana wawe na maisha kama wengine, wakipata fursa za kurekodi studio, wengine timu za kucheza mpira watafika mbali na kuliletea sifa taifa kutokana na vipaji vyao,"anasema.
Anaongeza: "Tunahitaji wafadhili wa kuwezesha yote hayo, Watanzania na wote wenye mapenzi mema tafadhalini wasaidieni vijana hawa warejee kwenye ujenzi wa taifa. Mimi nimeanza, nitakufa nao vijana hawa mpaka nikitoka Tanga, lakini tukumbuke kuwa vijana wasipokuwa na mwelekeo nchi haitatawalika."
Anaweka wazi kuwa anafanya yote hayo kwa kutumia fedha zake za mshahara, ingawa pia wapo wachache wanaomsaidia, akidokeza kuwa katika juhudi zake pia amewezesha vijana 200 wilayani humo kupata ajira.
Anawashukuru wasanii, Mzee yusuph aliyewachukua kijana mmoja, Tundaman watatu na Linex vijana watano kwa lengo la kusaidia kuwakuza katika sanaa ya muziki.
Dendegu ni mwenyeji wa Mkoa wa Morogoro na kwa maneno yake, anaeleza kwamba ametokea kwenye familia ya kawaida ya mkulima(Mzee Dendegu), aliyekuwa pia mwanasiasa.
Alipata yake ya msingi mkoani humo na baadaye Kilakala sekondari, Msalato na kumalizia Forest alipolazimika kurejea kufuatia kifo cha mama yake, aliyemwachia kazi ya kulea wadogo zake saba. Hata hivyo wawili kati yao sasa ni marehemu.
Dendegu ambaye ni mama wa watoto wawili mmoja wa kike, mwingine wa kiume alipata shahada yake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,(UDSM) kabla ya kuajiriwa na 'Foundation fo Civil Society mwaka 2003, ambapo alipata fursa ya kuzunguka mikoa yote nchini na kuwa karibu na jamii kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya mwaka 2012.
Akizungumzia ndoto zake kimaisha ni kusonga mbele zaidi kwa kujituma na kuweka utaifa mbele, huku akisema kuwa bado hajawa na ndoto ya kuwa mbunge kwani wajibu alionao sasa ni utumishi wa watu pia
0 comments:
Post a Comment