Monday, 19 August 2013

WATUHUMIWA WA DAWA ZA KULEVYA KUJIELEZA MBELE YA TUME



Madawa ya kulevya 

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA), Moses Malaki, amesema watuhumiwa wa njama za kupitisha kilo 150 za dawa za kulevya  aina ya Crystal Methamphetamine, watasimamishwa kazi wakati wowote kuanzia leo kabla ya kupewa nafasi ya kujitetea kwenye tume itakayoundwa kuwachunguza.
Hatua hiyo inatokana na agizo la Waziri wa Uchukuzi,  Dk Harrison Mwakyembe,  kutaka wote waliohusika na njama hizo kuchukuliwa hatua za kisheria.


Malaki ambaye awali alionyesha kushangazwa na kiasi kikubwa cha dawa hizo kupita, alisema utaratibu unakamilika wa kuundwa tume na kuwasimamisha kazi wahusika.


“Baada ya tume kukamilika na kupewa hadidu rejea, tutawaita mmoja mmoja kwenye   kujieleza, hapo tutajua kama wahusika watakuwa na hatia au la,” alisema.

Alisema baada ya kumaliza kazi, tume itatoa maelekezo kwa Serikali kinachotakiwa kufanyika.
Katika hatua nyingine,  jalada la mtuhumiwa wa dawa za kulevya aliyekamatwa JNIA Alhamisi iliyopita, akiwa na kete 84 na misokoto 34 ya bangi linapelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali leo.


Kamanda wa Polisi Vikosi cha Viwanja vya Ndege nchini, Deusdedit Kato, alisema jana kuwa wameshakamilisha upelelezi na kwamba,  wanasubiri maelekezo kutoka kwa Mwanasheria Mkuu.


Mtuhumiwa huyo alikamatwa JNIA mwishoni mwa wiki iliyopita, akiwa katika harakati za kusafirisha dawa hizo kwenda nchini Italia kupitia Zurich, Uswisi.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, kumekuja ikiwa ni siku moja baada ya Dk Mwakyembe kufanya ziara ya kushtukiza JNIA kukagua utendaji.

Na Bakari Kiango, Mwananchi  
Posted  Jumatatu,Agosti19  2013  saa 8:50 AM

0 comments: