JAJI wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Francis
Mutungi, ameteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Msajili wa Vyama vya
Siasa.
Taarifa ya uteuzi huo iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais, Ikulu na kutiwa saini na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni
Sefue, ilisema kuwa uteuzi huo ulianza Agosti 2, mwaka huu.
Jaji Mutungi anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Msajili wa
Vyama vya Siasa, John Tendwa, ambaye amestaafu utumishi wa umma kwa
mujibu wa sheria.
Uteuzi huo unamfanya Jaji Mutungi kuwa msajili wa tatu tangu kurejeshwa tena mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.
Aliyekuwa wa kwanza kukalia ofisi hiyo ya msajili ni Jaji mstaafu,
George Liundi, kisha akafuatiwa na Tendwa, ambaye amerithiwa na Jaji
Mutungi.
Jaji huyo aliwahi kuwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania.
Wapinzani wasifu
Kufuatia uteuzi huo mpya, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kimesema kuwa Tendwa alipaswa kuwa ameondoka ofisini tangu mwaka 2008
alipofikisha umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria.
Tarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uenezi ya chama hicho imesema kuwa
Tendwa alitumia muda huo wa miezi kadhaa alipoongezewa mkataba kuropoka
na kuharibu demokrasia kwa manufaa ya Rais Kikwete na CCM.
CHADEMA iliongeza kuwa kutokana na mwenendo wake mbovu, chama hicho
kilitangaza kutokumpatia ushirikiano wowote kwa vile alikuwa adui wa
demokrasia nchini.
“Kwa muda wote huo, CHADEMA ilikuwa ikitoa ushirikiano kwa Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa. Badala ya kuifuta CHADEMA na kufanikisha
dhamira ovu ya kuharibu amani ya nchi, ameondoka yeye,” ilisema taarifa
ya
CHADEMA.
CHADEMA ilisema kuwa wanamkaribisha Jaji Mutungi kwenye kazi na
majukumu yake mapya. Kwamba, wapenda demokrasia na maendeleo nchini
wanamtarajia atatimiza wajibu wake kwa kuzingatia haki, sheria na
utawala bora, asije akapita njia ya Tendwa.
“Kupitia mchakato wa Katiba mpya unaojadiliwa sasa hivi, CHADEMA
tunapendekeza Ofisi ya Msajili ipewe uhuru zaidi na uteuzi wake usiwe
suala la rais kuamka tu na kuamua kuteua bila wahusika kuomba, kuchujwa
na kuthibitishwa na mamlaka nyingine tofauti na iliyoteua,” walisema.
Jaji Mutungi, anapaswa kuonesha kwa maneno na vitendo kwamba hatakuwa
kama Tendwa, kwa kuanza kushughulikia matendo ya kiharamia yaliyofanywa
na Green Guards wa CCM kwenye chaguzi za madiwani zilizomalizika hivi
karibuni.
Naibu Mkurugenzi wa Uenezi na Haki za Binadamu wa Chama cha Wananchi
(CUF), Abdul Kambaya, alisema ni jambo zuri ingawa aliyemteua vilevile
ni Mwenyekiti wa CCM, hatua ambayo inaleta hofu kidogo.
“Tunadhani ni mtu mweledi, sisi hatupigi ramli kuhusu utendaji wake,
mpaka tutakapomwona akianza kazi. Wakati wa Tendwa tumefanya kazi katika
mazingira magumu, hasa sisi wapinzani, tunaomba huyu asifuate hayo.
Tendwa aliiogopa sana CCM,” alisema.
Naye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Sam Ruhuza, alisema wanamtakia kila
jema Tendwa na kumkaribisha kwa furaha Jaji Mutungi, japokuwa wateule
wote huwa wanafanya kazi ya kumpendeza aliyewateua.
|
0 comments:
Post a Comment