Baadhi ya wafanyakazi wa Tazara wakiwa nje ya ofisi ya mwajiri
WAFANYAKAZI wa Shirika la Reli ya TAZARA Mkoani
Mbeya wameingia katika Mgomo kwa muda usiojulikana wakishinikiza Uongozi wa
Shirika hilo kuwalipa mishahara yao ya Miezi mine(4).
Aidha watumishi hao wapatao zaidi ya 400 pia
wamemwomba Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuingilia mgogoro huo kwa kile walichodai
kuwa Ahadi ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe aliyoitoa Agosti 3,
Mwaka huu alipozungumza na wafanyakazi kuwa ameshindwa kuitekeleza.
Wakizungumza na waandishi wa Habari katika Ofisi
za Tazara zilizopo Iyunga Jijini Mbeya baada ya Maandamano yaliyoishia katika
Ofisi ya Mwajiri walisema Shirika hilo limeshindwa kuwalipa mishahara tangu
Mwezi May Mwaka huu na kusababisha Wafanyakazi kuishi maisha ya tabu.
Walisema madai yao yameanza muda mrefu hali
iliyopelekea Waziri Mwakyembe kufika na kuzungumza nao na kuahidi kuwa Ifikapo
Agost 22, Mwaka huu Menejimenti iwe imelipa mishahara ya watumishi wote ikiwa
ni pamoja na kukusanya madeni ya wateja wao yanayofikia Bilion 5.
Walisema hadi sasa hakuna kilichotekelezwa hali
iliyowalazimu kugoma kujishughulisha na kazi yoyote inayohusu Tazara hadi hapo
watakapolipwa Mishahara yao au Waziri Mkuu atakapoingilia na kutatua madai yao.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Tazara
kanda ya Mbeya (TRAWU), Christopher Kazio, alisema hali ya wafanyakazi ni mbaya
na inasababisha kuyumbisha usalama wa eneo husika kutokana na baadhi yao
kufukuzwa katika nyumba walizopanga kutokana na ukosefu wa fedha.
Alisema hali ya usalama nayo si shwari kutokana
na wafanyakazi kuanza kuiba baadhi ya vitu ili kujipatia chochote ili waweze
kumudu ugumu wa maisha unaotokana na ukosefu wa fedha kwa zaidi ya miezi minne
ambayo wafanyakazi wnalidai shirika.
Naye Mwenyekiti wa wafanyakazi wa Tazara Mbeya
Mjini Rafael Kazyoba, alisema Wafanyakazi wote kwa ujumla wamekubaliana
kutofanya kazi yoyote hadi hapo uongozi wa Tazara utakapoamua kuwalipa
mishahara yao na sio kutoa ahadi ambazo wameshindwa kuzitekeleza.
Aidha kwa upande wa kampuni ya ulinzi inayolinda
katika Stesheni ya Mbeya ya Kilumi Security nayo ikaibuka na kudai kuwa uongozi
wa Tazara haujali maslahi ya watu na kutekeleza mikataba inayotakiwa na kwamba
wao kama walinzi wanapata wakati mgumu wa kulinda usalama wa wafanyakazi walio
na njaa wakiwemo wao wenyewe.
Jemsi Malembeka ni Afisa Rasilimali watu wa
Kampuni hiyo ambaye alisema tangu waingie Mkataba wa kulindamaeneo ya Tazara
takribani Miezi 6 imepita hawajawahi kulipwa hali inayosababisha walinzi
kukimbia na wengine kujihusisha na wizi wa vitu vya Tazara.
Wakati madai ya wafanyakazi yakiendelea na huku
wakitangaza mgomo mengine mapya yakaibuka baada ya Wazee wastaafu na wajane wa
Tazara kukjitokeza na kudai kuwa tangu wastaafu kazi miaka ya 1993 Hadi 2003
hawajalipwa mafao yao.
Juvenary Ngaiza (mstaafu) na Aida
Mbunda(Mjane) walisema tangu kustaafu kwao Serikali, Tazara na mashirika ya
Pensheni yameshindwa kulipa stahiki zao kwa muda mrefu na wamekuwa hawatoi
majibu ya kueleweka.
Walisema ni vema mashirika hayo yakathamini
mchango walioutoa wakiwa wafanyakazi wao na siyo kuwasahau baada ya kustaafu
hali inayowapekea kunyanyaswa pindi wakianza kudai mafao yao ambayo ni haki
yao.
HABARI HII NI KWA HISANI YA Mbeya yetu BLOG
|
0 comments:
Post a Comment