Tuesday, 20 August 2013

KIONGOZI MKUU WA BRATHERHOOD AKAMATWA

 
Mohammed Badie
Kiongozi mkuu wa vuguvugu la Muslim Brotherhood nchini Misri, Mohammed Badie amekamatwa na maafisa wa usalama kutoka makaazi yake eneo la Nasr 'City', Mjini Cairo. Badie aliwekewa kibali cha kumkamata kwa tuhuma za kuchochea ghasia na mauaji.
Hali ya hatari imetangazwa Misri huku serikali ikiendelea kuwawinda wafuasi wa Brotherhood ambao wamepinga kuondolewa madarakani kwa Rais Mohammed Mosri.
Karibu watu 900 wameuawa wakiwemo mahabusu wa Brotherhood 37 ambao walifariki dunia wakipelekwa katika jela moja nje ya mji wa Cairo.Mamia ya wafuasi wa vuguvugu hilo akiwemo Naibu wake Badie, Khairat al-Shatir wamekamatwa tangu kuondolewa kwa Mohammed Mosri hapo Julai Tatu.
Mohammed Badie amekua akiwaomba wafuasi wa Muslim Brotherhood kuandamana na kuweka kambi zao mjini Cairo. Hata hivyo alikwenda mafichoni tangu Julai 10. Jeshi lilivunja kambi hizo na watu wengi waliuawa na kujeruhiwa.

Kiongozi huyo anakabiliwa na mashtaka ya kuchochea ghasia na mauaji ya raia wanane mahasimu wa Muslim Brotherhood.Kukamatwa kwa Badie kunajiri siku kadhaa baada ya mwanawe wa kiume Ammar kupigwa risasi na kuuawa katika maandamano yaliyofanyika medani ya Ramses.
Vuguvugu hilo limesema hatua ya kumkamata kiongozi wao hazitakandamiza wafuasi wake na kwamba mamilioni wataendelea kupinga mapinduzi dhidi ya utawala uliochaguliwa kidemokrasia.Mrengo wa Brotherhood wa kisiasa, mbacho ni chama cha Freedom And Justice umemtangaza Mahmoud Ezzat kuchukua nafasi ya kiongozi mkuu.

Ezzat ni Naibu mwenyekiti wa chama hicho. Wakati huo huo Misri imetangaza siku tatu za maombolezi ya kitaifa kufuatia mauaji ya maafisa 25 wa polisi katika Rasi la Sinai, hapo Jumatatu.
Wanamgambo wa kiisilamu wamelaumiwa kutekeleza mauaji hayo.Shambulio hilo lilifanyika katika mji wa Rafah ulioko mpaka na Ukanda wa Gaza.

0 comments: