Wednesday, 28 August 2013

KAULI ZA JAJI MUTUNGI NA TENDWA BAADA YA KUAPISWA MSAJILI WA VYMA VYA SIASA

Picture: Mutundi-Kikwete-Tendwa
 
Msajili mpya wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema kazi iliyoo mbele yake ni ngumu, hivyo ameomba apewe miezi mitatu aifahamu kwanza ofisi kabla ya kuueleza umma matarajio yake, ikiwa ni pamoja na namna atakavyoshughulikia changamoto zote zinazoikabili ofisi aliyokabidhiwa kuisimamia.

Jaji Mutungi alisema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi na wa habari, muda mfupi baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu, jijini Dar es Salaam juzi: “Mimi bado ni mgeni, nipeni muda niifahamu ofisi, najua kazi ni ngumu,” alisema Jaji Mutungi.

Alisema ugumu wa kazi katika ofisi hiyo, unatokana na matarajio ya jamii kwake kuwa makubwa, hivyo mategemo yake ni kupata ushirikiano kutoka kwa wadau, wakiwamo waandishi wa habari ili kufanikiwa kuzikabili changamoto hizo.

Hata hivyo, aliwahakikishia Watanzania kuwa kazi yake katika ofisi hiyo itakuwa ni kutenda haki tupu kama fani yake ya Uanasheria inavyomtaka atende: “Subirini nikiingia ofisini. Nipeni miezi mitatu,” alisema Jaji Mutungi.

Naye Msajili mstaafu wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, ambaye alihudhuria hafla ya kuapishwa kwa Jaji 
Mutungi jana, aliwataka Watanzania kumsaidia msajili huyo mpya kutenda mambo yote anayotarajia kuyafanya, kama vile kukuza demokrasia, ambayo alisema ndiyo msingi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Hata hivyo, Tendwa alisema kustaafu kwake siyo mwisho wa maisha, bali ni mwanzo wa maisha mengine mapya: “Ninawaaga Watanzania, ambao walikuwa wananiamini katika demokrasia. Mtu akikupiga madongo, usimrudishie atakuja kujuta,” alisema Tendwa na kuongeza: “Ukiona watu wengi wanakupigia makofi, jiulize je, wananipenda au wananipaka mafuta kwa mgongo wa chupa. Kama hawakutaki shukuru.”

Alisema anachojivunia katika kipindi chake cha miaka 13 cha uongozi wa ofisi hiyo, pamoja na mambo mengine, ni kusimamia utitiri wa vyama, ambavyo vingi vimekuwa vikiishi kwa migongano, lakini akafanikiwa kuviweka sawa.

Tendwa aliteuliwa aliteuliwa kushika wadhifa huo Aprili 27, 2001 akichukua nafasi ya George Liundi.

Wengine waliohudhuria hafla ya kuapishwa kwa Jaji Mutungi jana, ni Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman; Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue. Wengine ni Msajili Mkuu wa Mahakama, Ignas Kitusi; Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Hussein Katanga; pamoja na viongozi wakuu wa vyama vya siasa nchini. 

Jaji Mutungi aliteuliwa na Rais Kikwete kushika nafasi hiyo Agosti 2, mwaka huu. Anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Tendwa, ambaye amestaafu utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria. Kabla ya uteuzi huo, Jaji Mutungi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma.

--- Habari ya maandishi imenukuliwa kutoka kwenye gazeti la NIPASHE na picha kutoka IKULU.

 

0 comments: