Saturday, 24 August 2013

ALIYEGUSHI SAINI YA WAZIRI MKUU PETER PINDA APANDISWA KIZIMBANI

 
MFANYABIASHARA  Amadi Ally Popi (35), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikakabiliwa na makosa mawili likiwemo la kughushi barua inayoonyesha imeandikwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Inspekta wa Polisi Hamis Said mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alilitaja kosa la kwanza linalomkabili Popi ni la kughushi kinyume na kifungu cha  333,335(a) na 337 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Inspekta  Said alidai  kuwa tarehe na siku isiyofahamika ndani ya jiji la Dar es Salaam,  kwa nia ya 
kudanganya  Popi alighushi barua yenye kumbukumbu Na,DA21/3078/01A/142 ya Desemba 3 mwaka 2012 akijaribu kuonyesha  kuwa barua hiyo ni halali na ilikuwa imeandikwa na kusainiwa na  Waziri Mkuu  Pinda.

Said alilitaja kosa la pili kuwa  ni la kutengeneza nyaraka  ya serikali bila ya kuwa na mamlaka ya kufanya hivyo kosa ambalo ni kinyume cha kifungu cha  346(a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, ambapo tarehe na siku isiyofahamika ndani ya jiji la Dar es Salaam,
 Popi bila ya kuwa na mamlaka yoyote  alitengeneza barua hiyo na kuisani na kisha alimpatia barua hiyo Islamu Mohammed Mtila  akijaribu kuonyesha barua hiyo  imetoka katika ofisi ya waziri Mkuu na imesainiwa na Waziri Mkuu Pinda.

Hata hivyo mshitakiwa huyo alikanusha mashitaka yote na Hakimu Lema alisema ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima  awe na wadhamini wawili wanaofanyakazi serikali au kwenye taasisi zinazofahamika ambapo watasaini bondi ya Sh. milioni 10 na mmoja katika wadhamini hapo atawasilisha mahakamani hati ya mali isiyoamishika yenye thamani hiyo, masharti ambayo yalishindwa kutekelezwa na mshitakiwa huyo na hivyo hakimu Lema aliamuru mshitakiwa apelekwe rumande hadi Septemba 5 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya kutajwa na upepelezi wa shauri hiyo haujakamilika.

Imeandikwa na Happiness Katabazi, Tanzania Daima

 

0 comments: