Tuesday, 13 August 2013

MAJAJI WATATU NA JAJI KIONGOZI, WATASIKILIZA KESI DHIDI YA PINDA

  PICHA YA MH MIZENGO PINDA  ALIPO KUA BUNGENI
 
 
JAJI Kiongozi, Fakhi Jandu, anatarajiwa kuongoza jopo la majaji watatu watakaosikiliza kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) dhidi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,majaji wengine waliomo kwenye jopo hilo ni Jaji Augustine Mwarija na Dokta Fauz Twaib.

Hata hivyo tarehe ya usikilizaji wa shauri hilo bado haijapangwa. LHRC na TLS walimfungulia Waziri Mkuu Pinda, kesi hiyo kutokana na kauli yake aliyoitoa bungeni ya kuruhusu vyombo vya usalama kuwapiga watu wanaokataa kutii sheria zinazotolewa na mamlaka husika.Mbali na Pinda, mwingine aliyeunganishwa katika 
kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambapo kwa upande wa LHRC inawakilishwa na mawakili zaidi ya 20.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Waziri Pinda, anakabiliwa na tuhuma za kudaiwa
kuvunja Katiba ya nchi kwa kuruhusu askari kuwapiga wananchi.Mkurugenzi wa LHRC, Dkt. Hellen Kijo Bisimba wakati akifungua mashtaka hayo katika Mahakama Kuu alisema kuwawanamshtaki Waziri Mkuu kwa maelezo kuwa amekiuka kifungu cha Katiba Ibara 13 (1).

Pinda ametajwa kwenye hati hiyo akiwa mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo namba 24.

Naye Mjumbe wa Bodi ya LHRC, Wakili Dkt. Ringo Tenga alisema katika kesi hiyo wameangalia zaidi sheria na hasa haki za msingi za binadamu na kwamba kauli hiyo ya Waziri Mkuu Pinda inahatarisha haki hizo. Hata hivyo, hatua hiyo ya LHRC ilipingwa vikali na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Nchini (DPP), Dkt. Elieza Feleshi akisema hakuna uhalali wa mashtaka yoyote dhidi ya kiongozi huyo sababu kauli ya Pinda kuwa pigeni haikuwa piga ua. -- Rehema Mohamed, MAJIRA
 

 

 

0 comments: