Thursday, 22 August 2013

NSAJIGWA NA MWASYIKA KUISHTAKI YANGA TFF


  


WACHEZAJI wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Shadrack Nsajigwa na Stephano Mwasyika, wanajipanga kuishitaki klabu yao ya zamani kwa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), wakishinikiza walipwe Sh milioni 16 wanazoidai klabu hiyo. Nsajigwa, aliyemaliza mkataba wake kwenye klabu hiyo, anaidai Yanga Sh milioni 10, huku Mwasyika akidai Sh Milioni 6, jambo linalowafanya watangaze kulipeleka TFF suala hilo.

Wachezaji hao kabla ya kuondoka waliitumikia klabu ya Yanga kwa mafanikio makubwa na kufanikiwa kuchukua makombe mbalimbali, hasa lile la Afrika Mashariki na Kati ‘Kagame’, mwaka jana.


Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, alisema Yanga inawaomba wachezaji hao wawili, wasitishe nia yao, kwani watakuwa wanaidhalilisha Yanga.

“Tunatambua mchango wa wachezaji hao, hivyo hatuwezi kuwadhulumu fedha hizo, kama wamedhamiria kuidhalilisha Yanga, basi waache, malengo yetu ni kuwalipa kama sehemu ya kuheshimu kujitoa kwa moyo katika timu yao, hawa ni wachezaji wazuri na wamefanya kazi kubwa kuichezea Yanga, hivyo naomba tuseme kuwa fedha zao zitalipwa kwa wakati na tunaomba wasifike mbali kwa heshima ya klabu yetu.

“Awali tuliwaita klabuni Agosti 20 mwaka huu, kujadili namna ya kuwalipa fedha zao, lakini hawakutokea, licha ya kuwatafuta mara kadhaa, hivyo si jambo la busara kuanzisha mvutano usiokuwa na kichwa wala mguu,” alisema Mwalusako.

Yanga kwa sasa inajiandaa na kivumbi cha Ligi ya Tanzania Bara, huku wao wakiwa ndio mabingwa watetezi, baada ya kulitwaa msimu uliopita kutoka kwa Simba SC.

0 comments: