Tuesday, 6 August 2013

MAFUTA YAOK NAVIKING NI SALAMA SERIKALI YA ZANZIBAR IMESAEMA

Hafsa Golo na Asya Hassan — SERIKALI imesema mafuta ya kupikia ya OKI na Viking yako salama kwa matumizi ya binadamu.

Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi imefanya uchunguzi wa kina na kugundua kuwa mafuta hayo hayana tatizo na yanafaa kwa matumizi ya binadamu.

Alisema tangazo lililotolewa na Mamlaka ya Viwango Tanzania (TBS) kuwa mafuta hayo hayafai ni miongoni mwa mikakati ya kuua soko la wafanyabiashara wa Zanzibar.

Alisema baada ya uchunguzi huo alizungumza na Waziri wa Biashara wa Tanzania Bara na kumpa uthibitisho wa matokeo ya uchunguzi.

Alikuwa akijibu hoja mbali mbali za Wawakilishi baada ya kujadili na kuichangia bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

Kuhusu matumizi ya nembo ya TBS, alisema mamlaka hiyo inashindwa kudhibiti nembo yake hali
inayosababisha wafanyabiashara kuitumia vibaya hata kwa bidhaa zilizopitwa na wakati.

Aidha alisema TBS inakiuka sheria na taratibu huku ikikubali kutumiwa katika kudhoofisha biashara za Zanzibar kwa kuwalinda baadhi ya wafanyabiashara kwa maslahi binafsi huku wananchi wakiathirika na vyakula vilivyopitwa na muda.

Sambamba na hayo alikiri kwamba kuna baadhi ya wafanyabiashara wadanganyifu ambao wanaingiza bidhaa zisizo na kiwango na kughushi nembo.

Katika kupambana na wafanyabiashara hao, alisema wizara imekusudia kuongeza kikundi kazi cha kufuatilia kwa kina na kuhakikisha wanadhibitiwa.

Aidha alisema mradi wa kiwanda cha maziwa cha kampuni ya Azam una umuhimu mkubwa katika taifa ambapo utawezesha kutoa fursa mbali mbali za ajira nchini na kuinua ya uchumi wa wafugaji.

"Muekezaji huyu ana malengo mazuri hivyo ni vyema tukampa mashirikiano aweze kufikia dhamira ya kuleta maendeleo nchini, ikiwa mataifa mengine yanamuhitaji," alifahamisha.

Kuhusu kiwanda cha sukari Mahonda, Mazrui alisema kiwanda hicho kipo katika hatua zuri na mwishoni mwa mwaka huu kitaanza uzalishaji wa sukari.

Akizungumzia mzozo baina ya kiwanda hicho na wakulima wa mpunga katika mashamba yanayomilikiwa na kiwanda, alisema hana taarifa lakini aliahidi kufuatilia kwa kushirikana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya
Kaskazini ‘B’.

Nae Naibu Waziri, Thuwaiba Edington Kisasi alisema wizara ina lengo ya kurudisha maonesho ya biashara ili kuitangaza Zanzibar kibiashara.

Alisema serikali imetenga eneo katika kijiji cha Dimani na kinachofanywa ni kuboresha miundombinu ya barabara na huduma za maji na umeme.

Bajeti ya wizara hiyo ilipitishwa juzi.

--- Rejea ya habari: ZanziNews.com
 

 

0 comments: