Monday, 12 August 2013

DIWANI AWEKA TAA ZA BARABARANI NA MBUGE AGAWA KOMPYUTA 28

Moshi — DIWANI wa Longuo B, Raymond Mboya (CHADEMA), amejitolea kuweka taa kwenye barabara za Mtaa wa Kitandu ambao upo karibu na Hospitali ya Rufaa ya KCMC baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kufanyiwa vitendo vya ubakaji na wizi.

Diwani Mboya alisema alipokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi wa udaktari wanaosoma KCMC kwenye mkutano alioufanya Juni mwaka huu juu ya kuwapo kwa matukio hayo. Alisema waliweka ulinzi jamii, lakini ilionesha kutozaa matunda hivyo kuamua kuweka nguzo pamoja na taa kwenye barabara ya mtaa huo.

Mmoja wa wananchi wa Mtaa wa Kitandu akizungumza na Tanzania Daima, Alex Mbaga alisema vitendo vya 
wizi vilikuwa vimekithiri kutokana na barabara hizo kutokuwa na taa za barabarani na kuwa na giza, hivyo majambazi kutumia nafasi hiyo kuwaibia watu. Alisema kwananchi waliokuwa wahanga wa matukio hayo ni wanafunzi wanaosoma udaktari kwenye Chuo cha KCMC, wale wa Ushirika (MUCoBS) pamoja na Mwenge ambao wamepanga nje ya vyuo kwenye mtaa huo. (Rodrick Mushi, Moshi — TanzaniaDaima)
---

Mbunge agawa kompyuta 28 jimboni mwake

Babati — MBUNGE wa Jimbo la Babati Vijijini, mkoani Manyara, Vrajilal Jituson kupitia Mfuko wa Ofisi yake ameazimia kutoa kompyuta mpakato 28 kwenye maeneo tofauti ya jimbo lake kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi wa taasisi mbalimbali.

Jituson ambaye ni Mwanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa huo, (MAMEC) alisema alitoa kompyuta mbili mpakato (laptop) kwa ajili ya waandishi wa habari wa mkoa huo, ili waweze kuandika habari za vijijini.

Akizungumza jana mjini Babati, mbele ya Rais wa Muungano wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Keneth Simbaya, mbunge huyo alisema amejitolea kompyuta hizo kwa lengo la kurahisisha teknolojia ya mawasiliano: “Pamoja na kuwapa waandishi wa habari hizo laptop mbili pia tumetoa laptop mbilimbili kwenye vituo vya polisi vya mjini Babati na Magugu ili waweze kusaidia jamii kuandika taarifa zao,” alisema Jituson.

Alisema katika kompyuta hizo 28, amepanga kugawa kompyuta tano kwa kila tarafa ili zipelekwe kwenye shule za sekondari, kwani lengo lake ni kila shule ya sekondari katika kata ipate kompyuta yake.

Kwa upande wake, Simbaya alipongeza hatua ya mbunge huyo kugawa kompyuta hizo kwa waandishi wa habari kwani amekuwa tofauti na wabunge ambao wanawathamini waandishi kwenye kipindi cha uchaguzi pekee. (MWANANCHI)
 


0 comments: