Saturday 1 June 2013

CWT YASISITIZA MGOGORO WAKE NA SERIKALI BADO MBINCHI


Rais wa CWT Gration Mukoba
Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimesema mgogoro kati yake na serikali bado uko pale pale kwa kuwa hawajafikia muafaka wa mazungumzo yao.

Chama hicho ambacho kinaidai serikali zaidi ya sh. bilioni 25, kimeeleza kuwa mbali ya kuwepo kwa vikao kadhaa kati ya chama hicho, lakini hakuna muafaka uliofikiwa.


Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Rais wa CWT Gration Mukoba, alisema amelazimika kuyasema hayo ili wabunge waelewe kabla ya bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi haijasomwa Bungeni wiki ijayo.


“Mgogoro wa walimu na serikali umepoa kwa muda tu. Wajue ngoma ya walimu na serikali bado ni mbichi. Hatujafikia muafaka…” alisema Mukoba.


Rais Mukoba alisema wapo walimu waliopanda madaraja muda mrefu, lakini hadi sasa mshahara wanaopata ni wa zamani.


Kwa mujibu wa Mukoba, maamuzi ya nini CWT itafanya yatatolewa mwezi ujao baada ya Baraza la Walimu kukutana.


Alisema hata nyongeza ya mishahara iliyotangazwa na serikali, haihusiani na madai yao.

Akizungumzia mkutano wa mwisho ulioitishwa na Baraza la Majadiliano kati ya Mei 24 na 25 mwaka huu, Rais wa CWT alisema, CWT iliomba serikali kuwapandishia mshahara walimu kwa asilimia 100 lakini serikali ilipinga.

“CWT ilishuka kutoka asilimia 100 hadi 65 wakati serikali ilipanda kutoka asilimia 12.09 hadi 24.19. Baada ya kufikia asilimia 24.19 serikali iliripoti kuwa uwezo waliopewa wa kujadiliana (Mandate) ulikuwa umeisha wakati CWT walikuwa bado wanauwezo wa kuendelea na mjadala kulingana na ‘Mandate’ waliyokuwa wamepewa,” alisema.


Alisema kutokana na hali hiyo, wajumbe wa serikali waliomba muda wa kwenda kujadiliana na wakubwa wao waliowatuma.


CWT mwezi Mei mwaka jana ilitangaza mgomo ambao Mukoba alisema hauku zaa matunda kwani serikali ilikimbilia mahakamani.


Alisema mahakama iliusitisha ambapo pamoja na mambo mengine iliagiza CWT na Serikali kukutana kwenye meza ya mazungumzo.


Baadhi ya madai ya msingi ya walimu ni ongezeko la mishahara kwa asilimia 100, kurudishwa kwa posho ya kufundishia (Walimu wa sayansi asilimi 55 na wa sanaa asilimia 50) na posho ya asilimia 30 kwa walimu wanaofanya kazi katika mazingira magumu.


Alisisitiza kwamba ni ukweli usiopingika kuwa kufufua mioyo hiyo kutafufua utendaji wao na hivyo kuboresha elimu ya Tanzania kwa maslahi ya sasa na baadaye.




 
SOURCE: NIPASHE

0 comments: