TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Jana tarehe 16/07/2014 Kamati Kuu
ya Halmashauri Kuu ya CCM ilifanya kikao cha kawaida cha siku moja
mjini Dar es salaam. Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Dr.
Jakaya Mrisho Kikwete.
Pamoja na mambo mengine kikao
hicho kilipokea taarifa ya mazungumzo yanayoendelea kati ya CCM kwa
upande mmoja na CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kwa upande wa pili.
Mazungumzo hayo yanayosimamiwa na
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi yana lengo la
kuangalia kwa kina ni kwa nini baadhi ya wajumbe wachache wa Bunge
Maalum la Katiba walisusia na kutoka nje katika awamu ya kwanza ya Bunge
hilo, na kuangalia namna watakavyorudi ili kukamilisha mchakato wa
mabadiliko ya Katiba nchini.
Kwa ujumla Kamati Kuu ya CCM
imeridhishwa na mwenendo wa mazungumzo hayo na kupongeza juhudi hizo
zilizofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa na Vyama husika. Kamati Kuu
inapenda kueleza imani yake kuwa mazungumzo hayo yatazaa matunda kwa
wajumbe wachache waliosusia Bunge Maalum la Katiba, kurejea Bungeni na
kumalizia sehemu ya mchakato uliobakia. Kamati Kuu inayatakia kila la
kheri mazungumzo hayo.
Kamati Kuu pia ilipokea taarifa
za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonesha nia ya kuomba
ridhaa ya CCM kugombea Urais. Baada ya kutafakari kwa kina, Kamati Kuu
inapenda kuwakumbusha wote kuwa ili wasipoteze sifa za kugombea, ni
muhimu wakazingatia Katiba, Kanuni na taratibu za Chama zinazosimamia
masuala hayo.
Kuhusu wale waliopewa adhabu na
Kamati Kuu kutokana na kukiuka baadhi ya taratibu za Chama kwa suala
hili, Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama itafanya mapitio ya mwenendo
wao wa utekelezaji wa adhabu hiyo mwezi wa nane (Agosti 2014), na kama
itabainika kuwa hawatekelezi ipasavyo masharti ya adhabu zao,
itapendekeza kwa Kamati Kuu kuongezwa kwa adhabu kulingana na ukubwa wa
uvunjaji wa masharti ya adhabu husika.
Ni muhimu wanachama wote
wakakumbuka kuwa Chama ni pamoja na Katiba, Kanuni na taratibu zake,
hivyo kutoziheshimu na kuzifuata ni kukivuruga, jambo ambalo
halivumiliki.
Nia ya CCM kusimamia haya ni
kuhakikisha Chama kinakuwa na umoja na mshikamano ambao ni muhimu sana,
hasa tunapoelekea kukamilisha kazi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya 2010/2015 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Aidha, Kamati Kuu imewatakia kheri na fanaka Watanzania wote wakati huu wanapomalizia mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Aidha, Kamati Kuu imewatakia kheri na fanaka Watanzania wote wakati huu wanapomalizia mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Imetolewa na:-
Nape M. Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
17/07/2014
0 comments:
Post a Comment