Saturday 26 July 2014

KOCHA WA ZAMANI STARS ASEMA KIKOSI CHA NOOIJ KITAING'OA MSUMBIJI


Imechapishwa Julai 26, 2014, saa 6:53 mchana

Aliyewahi kuwa Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Sylvester Marsh, amesema uwezo ulioonyeshwa na timu hiyo katika mechi yake dhidi ya Msumbiji ni mkubwa na anaamini itashinda katika mchezo wa marudiano.
Stars ilikutana na Mambas ya Msumbiji wiki iliyopita katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika inayotarajiwa kufanyika mwakani nchini Morocco ambapo katika mchezo wa awali, ilifanikiwa kutoka sare ya mabao 2-2.
Mambas ni moja kati ya timu ambazo zimekuwa zikiisumbua Stars kwa muda mrefu pindi zinapokutana nayo.
Marsh amesema kuwa mwenendo wa timu hiyo kwa sasa ni mzuri kufuatia maandalizi waliyoyafanywa na kuwataka Watanzania wasiwe na haraka ya kupata mafanikio, kwani hali hiyo hutokea hata katika maisha ya kawaida.
“Uwezo wa Stars kwa sasa upo juu ya Mambas kwa jinsi nilivyowaona walivyocheza katika mechi ya kwanza licha ya kutoka sare, hivyo nina imani kubwa kuwa itashinda na kuitoa katika mchezo wa marudiano.
“Tumeweza kuona katika mchezo wa awali tulifanikiwa kuitoa Zimbabwe licha ya kuwa na matokeo mabaya ya awali katika uwanja wa nyumbani.
“TFF imejitahidi kwa kiasi kukubwa kuiandaa timu hiyo kwa kukaa kambi kwa muda mrefu na kuipeleka nje ya nchi kwa ajili ya kujiandaa pamoja na kucheza mechi za kirafiki, ambapo imebadilika kwa kiasi kikubwa, hivyo ni vyema wadau wakawa na subira kuhusiana na suala hilo ili timu iweze kufanya vizuri hapo baadaye,” alisema Marsh.

Chanzo: Salleh Ally

0 comments: