Saturday 1 June 2013

WANAFUNZI UWELENI PEMBASEKONDARI WACHAGAWA NA MASHETANI

  -- UONGOZI wa skuli ya sekondari ya Uweleni Pemba, umelazimika kuwazuiya wanafunzi wote wasiende skuli kwa siku ya pili sasa baada ya wanafunzi kuendelea kuchangawa mashetani.

Vituko hivyo vinajiri baada ya skuli hiyo kufanyiwa ukarabati mkubwa na tokea wanafunzi waanze kuyatumia madarasa ‘mapya’ wamekuwa wakikumbwa na mkasa huo na kusababisha tafrani kubwa kiasi kwamba walimu wanashindwa kufundisha kwa utulivu.

Juzi Jumatano (jana), uongozi wa skuli ulilazimika kuwarejesha makwao, wanafunzi wote baada ya hali ya hali kuwa mbaya huku wanafunzi wakianguka na kupiga kelele hovyo huku wengine wakitimua mbio.

Kutokana na tafrani hiyo, Kamati ya Uongozi ya skuli hiyo ilikutana na wazazi wa wanafunzi jioni ya juzi na 


kuamua wanafunzi hao waendelee kubaki majumbani mwao huku ufumbuzi wa kadhia hiyo ukitafutwa.

Baadhi ya wazazi na wanafunzi wa skuli hiyo, wameihusisha hali hiyo na imani za kishirikina, ambapo wamesema kabla ya kufunguliwa tena skuli, ilibidi kutolewe kafara kwa kuchinjwa ngo’mbe.

Hata hivyo kuna tetesi kuwa, matukio hayo yana mkono wa baadhi ya wananchi, ambao walitaka kabla ya skuli hiyo kufunguliwa achinjwe ng’ombe kwanza kitendo ambacho hakikufanyika.

Mwenyekiti wa kamati ya skuli hiyo, Maalim Hemad Ali alisema hali ya wanafunzi kuchagawa iliyojitokeza skulini hapo ni ya kutisha na inaweza kuhatarisha maisha ya wanafunzi, walimu na skuli kwa ujumla.

“Hali ni ngumu, wanafunzi wanapiga makelele ya kutisha, wanajirusha na kujipiga na chini na wengine kufikia hadi kuvua nguo,” alisema kwa huzuni .

Mmoja ya wazazi wa wanafunzi, Kassim Muhammed alitoa ushauri kwa kamati ya skuli na wazazi wenzake kuanzishwa kamati maalum ya wazee wa vijiji wanavyotoka wanafunzi ili kutafutwa undani wa tatizo hilo na kupatiwa ufumbuzi.

Alisema kuundwa kwa kamati hiyo kutarahisisha kuelewa kwa urahisi chanzo cha tatizo na kulipatia ufumbuzi.

Naye Ali Abas Omar alisema isicheleweshwe kutafutwa ufumbuzi kwani wanafunzi wanakosa masomo hali inayoweza kuwaweka katika mazingira mabaya.

Rais wa serikali ya wanafunzi wa skuli hiyo, Nizar Fesal alisema tatizo la kuchagawa linarejesha nyuma maendeleo ya skuli na wanafunzi kwani wanakosa vipindi vya masomo.

Nae mwanafunzi Fatma Salum, ameishauri jamii kujali maendeleo ya watoto wao na kuachana na masuala ya kishirikina.

Alisema jamii haina budi kufurahia ukarabati wa skuli hiyo badala ya kuchukia na kuanza kuwadhuru wanafunzi.
 habari na
  Habiba Zarali, Pemba (  ZanziNews blog)

0 comments: