Sunday, 8 June 2014

ULIMWENGU AISAIDIA TP MAZEMBE KUSHINDA 1-0 DHIDI YA ZAMALEK,


BAO pekee la Mzambia Rainfrod Kalaba dakika ya 13 limeipa ushindi wa 1-0 Tout Puissant Mazembe Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, DRC katika mchezo wa Kundi A, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri jioni hii. Mshambuliaji Mtanzania, Mbwana Ally Samatta hakuwemo kabisa katika orodha ya wachezaji walioshiriki mchezo wa leo kwa sababu bado majeruhi. Lakini Mtanzania mwenzake, Thomas Emmanuel Ulimwengu aliingia dakika ya 65 kuchukua nafasi ya Kalaba na akakaribia kufunga mara mbili.
Thomas Ulimwengu aliingia kipindi cha pili TP Mazembe ikiilaza 1-0 Zamalek
Ushindi huo, moja kwa moja unaipandisha kileleni mwa kundi hilo Mazembe, baada ya kufikisha pointi sita kutokana na mechi zote tatu za mzunguko wa kwanza. Katika mechi zake mbili za kwanza, Mazembe ilifungwa 1-0 na El Hilal ya Sudan kabla ya kushinda 1-0 dhidi ya ndugu zao, As Vita ya Kinshasa, DRC bao pekee la Samatta.  Baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na AS Vita jana, Hilal inafungana kila kitu na timu hiyo ya DRC, pointi nne na wastani sawa wa mabao ya kufunga na kufungwa, kila timu imefunga mabao matatu na kufungwa matatu. Zamalek inamaliza mkiani mwa kundi hilo kwa pointi zake tatu. Mzunguko wa pili wa Ligi ya Mabingwa unatarajiwa kuanza baada ya Kombe la Dunia Julai. 
 
Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM

0 comments: