Saturday, 21 June 2014

Wanamgambo wahimizwa kujitolea Iraq


  Jeshi la Mehdi mjini Najaf
Maelfu ya wanamgambo wa Kishia waliobeba silaha, wamefanya mhadhara mjini Baghdad na miji mengine ya Iraq ili kuonesha nguvu zao dhidi ya wapiganaji wa Kisunni ambao wameteka maeneo makubwa kaskazini mwa Iraq.
Wafuasi hao wa kiongozi wa Kishia mwenye msimamo mkali, Moqtada al-Sadr, piya walipinga wanajeshi wa Marekani kurudi Iraq kupambana na wapiganaji.
Kikosi cha Moqtada al-Sad kiliwahi kupigana na Marekani nchini Iraq kwa miaka kadha.
Katika mhadhara uliofanywa Kirkuk, mwakilishi wa Moqtada al-Sad, Raad al Sakhri, alihutubia wafuasi wa jeshi lao liitwalo Mehdi:
"Tunawahimiza muwe tayari kujitolea mhanga kuilinda nchi yetu tunayoipenda!"
Wapiganaji wa Kisunni wanaopambana na jeshi la serikali kaskazini mwa Iraq wanasema wameuteka mji wa Al-Qaim, karibu na mpaka wa Syria, kutoka mikono ya serikali.
Al-Qaim ni mji muhimu katika kuvuka mpaka ambao unaweza kuwaruhusu wapiganaji wa kundi la ISIS kupitisha silaha nzito, kutoka maeneo ya Syria wanayodhibiti, hadi Iraq.
Kundi hilo piya limesema kuwa limeuteka mji wa Rawa.
Na limeeleza kuwa mapambano makali yanaendelea kwenye kinu kikubwa kabisa cha kusafisha mafuta nchini Iraq, Baiji, na wamedungua helikopta mbili za serikali.

0 comments: