MWENYEKITI wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC, Wakili Dk Damas Daniel Ndumbaro amesema kwamba uamuzi wowote dhidi ya mgombea Urais wa klabu hiyo, Michael Richard Wambura hautokani na chuki binafsi.
Dk Ndumbaro ameiambia BIN ZUBEIRY jana mjini Dar es Salaam kwamba, hakuna msuguano wowote, baina yake na Wambura na maamuzi yote yanayomuumiza mgombea huyo, si yake binafsi, bali ya Kamati.
Ikumbukwe Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC ilimuengua Wambura kwa sababu alikiuka Katiba kwa kuipeleka klabu hiyo Mahakamani, jambo ambalo FIFA inakataza.
Wana bifu? Dk Ndumbaro kulia amesema hana chuki na Wambura kushoto |
Wambura alikata rufaa, Kamati ya Rufani ya TFF chini ya Mwenyekiti Wakili Julius Lugaziya, ambako alishinda na kurejeshwa kwenye kinyang’anyiro. Wakili Lugaziya alisema Kamati yake iliamua kumrejesha Wambura kwa sababu baada ya kosa alilolifanya aliendelea kuhudhuria mikutano ya klabu, kulipia ada zake za uanachama na pia akateuliwa katika Kamati ya Utendaji, iliyounda Kamati ya Uchaguzi ya sasa chini ya Ndumbaro.
Lakini jana, Ndumbaro baada ya ripoti ya Wakili Lugayiza alisema amemuengua tena Wambura kwa sababu amekiuka kanuni za uchaguzi kwa kufanya kampeni kabla ya muda
“Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC ilijadili kuhusu vitendo vya wagombea kupiga kampeni kabla ya muda wa kampeni ulioruhusiwa. Kwa mujibu wa Mchakato wa Uchaguzi ya Simba Sports Club, muda wa kampeni unaanza tarehe 24 -28 Juni 2014,”. “Hapo awali kamati ilibaini kuwa wagombea wawili wa nafasi ya urais; Michael Richard Wambura na Evans Aveva walifanya vitendo vya kampeni siku ya kuchukua na kurejesha fomu za kugombea. Tarehe 25 Mei 2014, Kamati iliwapa ONYO KALI la maandishi wagombea hao na kuwataarifu kuwa hatua kali zaidi zitachukuliwa dhidi yao, ikiwemo kuondolewa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi,”.
“Baada ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club kumuondoa Bw. Michael Richard Wambura katika kinyang’anyiro cha uchaguzi Mkuu wa SImba SC, Bw. Wambura aliitisha Mkutano na waandishi wa habari, aliitukana Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC na kutoa matamshi ambayo ni Kampeni,”.
“Baada ya ya Kamati ya Rufaa ya uchaguzi ya TFF kumrejesha Bw. Wambura katika Kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Simba, Bw. Wambura aliitisha tena mkutano wa waandishi wa habari, aliisifu kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF, kwa mara kwanza aliisifu Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC na kutoa matamshi ambayo ni wazi kuwa ni kampeni. Baadhi ya Matamshi aliyoyatoa kupitia vyombo vya habari ni kama ifuatavyo: “Simba Sports Club inahitaji zaidi wadhamini na sio wafadhili. Wafadhili kazi yao in kutoa fedha mfuko wa kushoto na kuepeleka mfuko wa kulia. Simba ilikuwa na viwanja vitatu lakini kimoja kimeuzwa na wajanja na vimebaki viwili tu,”.
“Kamati ya Uchaguzi ya Simba ilitafakari matamshi hayo, na kubaini kuwa hiyo ni kampeni ya waziwazi wakati muda wa kampeni bado haujaanza. Kamati ya Uchaguzi ya Simba ililipa jambo ili uzito wa kipekee kwa sababu Mkosaji amekuwa na tabia ya kurudia kosa hilo hata baada ya kupewe onyo la maandishi,”.
“HIVYO BASI: Kwa mujibu wa mamlaka ya kikanuni, hususan Ibara za: 6 (1) (a) – (g); 6 (1) (L) na 14(3) za Kanuni za uchaguzi za TFF – 2013, Bw. Michael Richard Wambura anaondolewa Katika Kinyang’anyiro cha Uchaguzi wa Simba SC, 2013, kwa kosa la kurudia kufanya kampeni kabla ya muda wa kampeni ambao umepengwa,”alisema Ndumbaro jana.
Akizungumzia maamuzi yake ya jana, Ndumbaro alisema kila anachosema ni maamuzi ya Kamati na si yake.
Lakini awali, katika vikao vyake Ndumbaro aliwahi kusema anafahamu udhaifu wa kitaaluma wa Wambura kwa kuwa ni mwanafunzi wake, jambo ambalo lilianza kuleta tafsiri kwamba, wawili hao wana chuki binafsi.
Wawili hao wote wameshitakiana Kamati ya Maadili ya TFF kwamba kila mmoja alimtukana mwenzake, ingawa TFF imegoma kusikiliza kesi hizo na kuamuru Simba SC iunde Kamati ya Maadili, wakati Ndumbaro amesema atazipelekea kesi hizo FIFA.
“Mimi sijawahi kumtukana Wambura, yeye alipokuwa anazungumza na Waandishi wa Habari, alihoji PhD yangu akisema ni feki, sasa mimi kusema nafahamu udhaifu wake wa kitaaluma kwa kuwa ni mwanafunzi wangu, si tusi, nilikuwa namjibu,”amesema Ndumbaro.
Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
0 comments:
Post a Comment